Na Baby Akwitende, Tanga
YANGA SC imekula ngwala katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Hadi mapumziko tayari Mgambo JKT walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Fully Maganga dakika ya kwanza tu ya mchezo akimalizia pasi ya Bashiru Chanacha.
Lilikuwa ni shuti la ghafla alilofumua mchezaji huyo mara tu baada ya kupata pasi, ambalo lilimkuta kipa Juma Kaseja akuiwa hajajiandaa kuokoa na kumpita kiulaini.
Hawa Mgambo hawafai; Kocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm leo amefungwa 2-1 na Mgambo Tanga
Mgambo ilipata pigo dakika ya 30 baada ya mchezaji wake, Mohamed Neto kutolewa nje kwa kadi mbili za njano, ya kwanza akikataa kukaguliwa na refa Alex Mahagi na ya pili kuzozana na refa huyo akipinga kusachiwa kama amebeba hirizi.
Dakika ya 32 kipa wa Mgambo, Saleh Tendega aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Tony Kavishe.
Kipindi cha pili Yanga SC walirudi kwa nguvu na kufanikiwa kusawazisha bao kwa penalti dakika ya 52 kupitia kwa Nahodha wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, baada ya bi wa Mgambo kuunawa mpira katika eneo la hatari.
Mgambo walicharuka baada ya bao hilo na kuanza kushambulia mfululizo langoni mwa Yanga na dakika ya 63 wakapata bao la ushindi.
Bao hilo lilifungwa kwa penalti na Malimi Busungu baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Yanga SC, Kevin Yondan.      
Matokeo hayo yanaifanya Azam iendelee kubaki kileleni kwa pointi zake 53 baada ya mechi 23, wakati Yanga SC inabaki na pointi zake 46 baada ya mechi 22.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva/Hamisi Kiiza dk77, Hassan Dilunga, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa/Hussein Javu dk61 na Emmanuel Okwi. 
Mgambo JKT; Saleh Tendega/Tony Kavishe dk32, Salim Mlima, Salim Gilla, Bashiru Chanacha, Bakari Mtama, Novatus Lukunga, Mohammed Samatta, Peter Mwalyanzi/Awadh Yassin dk88, Mohamed Neto, Fully Maganga na Malimi Busungu. 
CHANZO: BIN ZUBEIRY Blog
Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
AZAM FC imezidi kupiga kasi katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni hii kukiagusha kigogo, SImba SC kwa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Azam itemize pointi 53 baada ya mechi 23, wakati Yanga SC inabaki na pointi zake 46 baada ya mechi 22.
Shujaa; Mfungaji wa bao la ushindi la Azam FC kulia akipiga shuti pembeni ya kiungo wa Simba SC, Jonas Mkude
Shukrani kwake mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga bao la ushindi dakika ya 56 kwa kichwa kufuatia pasi ya tika tak ya Kipre Herman Tchetche. 
Tayari timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1 hadi mapumziko, Azam FC wakitangulia kupata bao lao kupitia kwa Khamis Mcha Vialli dakika ya 16 na Simba SC wakisawazisha kupitia kwa Joseph Owino dakika ya 45 na ushei.
Mcha alifunga bao kwa urahisi baada ya kutengewa mpira kwa kifua na Kipre Tchetche aliyepokea krosi Gardiel Michael- ambaye naye alipata pasi ya John Bocco aliyefanya kazi kubwa ya kupanda na mpira kutokea nyuma.
Owino alifunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na winga machachari, Ramadhani Singano ‘Messi’.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Henry Joseph/Abdulhalim Humud dk66, Haruna Chanongo, Amisi Tambwe, Uhuru Suleiman na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Aggrey Morris, David Mwantika, Kipre Balou, Himid Mao/Bryson Raphael dk75 , Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche/Brian Umony dk80 na Khamis Mcha ‘Vialli’/Kevin Friday dk55.
CHANZO: BIN ZUBEIRY Blog
Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
BONDIA Thomas Mashali amefanikiwa kutwaa taji la WBO uzito wa Light Heavy baada ya kumshinda kwa pointi Japhet Kaseba usiku wa jana kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba, Temeke mjini Dar es Salaam.
Majaji wote watatu walimpa ushindi bondia wa Manzese wa pointi 97-93 dhidi ya mbabe wa Kinondoni baada ya pambano hilo la raundi la 10, ambalo lilimalizika bila mtu kuanguka chini hata kwa sekunde wala kuhesabiwa kwa kuleweshwa ngumi.

Mshindi juu; Thomas Mashali akiwa amebebwa juu na mashabiki wake baada ya kutangazwa mshindi dhidi ya Japhet Kaseba

Kaseba aliyepanda ulingoni na mbwembwe nyingi, alianza vibaya katika raundi mbili za kwanza kabla ya kusimama imara katika raundi ya tatu na kumsukumia makonde mazito mpinzani wake.
Kaseba alirudi kwa kujiamini raundi ya nne na kumtandika mpinzani wake katika raundi yote hiyo. Hata hivyo, Mashali alizinduka raundi ya tano na kumdhibiti mpinzani wake, akianza kurusha ngumi za mbali na kuhama upande haraka.
Raundi ya sita, Kaseba aliingia na maarifa ya kupiga na kukumbatia hatimaye kufanikiwa kumpunguza kasi Mashali.
Kaseba alifanya vizuri katika raundi ya saba na ya nane, lakini Mashali akazinduka raundi ya tisa na kumalizia ya 10 pia vizuri.

Thomas Mashali kulia akipambana na Japhet Kaseba kushoto

Japokuwa hata matokeo yangetangazwa sare kusingekuwa na malalamiko, lakini Japhet aliridhia uamuzi wa majaji na kumkumbatia Mashali baada ya pambano.
Pamoja na ushindi, lakini Mashali hakucheza katika kiwango chake kiasi cha kumaliza raundi 10 na rasta mwenzake huyo ambaye kwa sasa anacheza ngumi kwa kulazimisha tu, kwani uwezo uliofanya akaitwa ‘Champ’ umekwishamkimbia. 

Bingwa na mataji; Thomas Mashali akiwa na mikanda yake baada ya kumshinda Japhet Kaseba
Katika mapambano ya utangulizi, Alan Kamote alimshinda kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya tano Karage Suba na kutwaa ubingwa wa UBO uzito wa Light, pambano kati ya Freddy Sayuni na Rajab Maoja lilivunjika raundi ya nne baada ya Maoja kuchanika na kushindwa kuendelea kugombea ubingwa wa PST.  
Said Mundi alimpiga Jumanne Mohamed kwa pointi pambano la uzito wa bantam, Issa Nampepeche alimpiga kwa pointi Zuberi Kitandula uzito wa bantam pambano lisilo la ubingwa, Saidi Chaku alitoka sare na Jocky Hamisi pambano la Feather lisilo la ubingwa na Majid Said alimpiga kwa pointi Frank Zaga uzito wa bantam pambano lisilo la ubingwa pia.

CHANZO; BIN ZUBEIRY BLOG (bongostaz.blogspot.com)

Nelson Mandela aaga dunia

 5 Disemba, 2013 - Saa 22:30 GMT
Rais wa zamani wa Afrika Kusini ameaga dunia . Mandela ameaga akiwa na umri wa miaka 95 na yeye ndiye aliongoza Afrika Kusini kutoka mikononi mwa watawala wa enzi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini baada ya kufungwa jela kwa miaka 27
Mandela alikua anpokea matibabu ya homa ya mapafu nyumbani kwake baada ya kulazwa hospitalini kwa miezi mitatu.

Mnamo mwaka 2005, Mandela alitangaza kwa taifa kua mwanawe wa kume alifariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.Katika taarifa yake kwa watu wa Afrika Kusini, Rais wa taifa hilo, Jacob Zuma , alisema kuwa Mandela amewaaga lakini yuko mahali salama.
Rais Zuma amesema kuwa taifa limepoteza mtu waliyemjua kama mtoto wa taifa hilo.
Mandela aliwahi kushinda tuzo ya amani ya Nobel, na kutambulika kama rais aliyeheshimika sana hasa kwa kupatanisha watu wa Afrika Kusini baada ya kuondoka gerezani.
Hakuonekana sana hadharani tangi alipostaafu mwaka 2004.
Na Mahmoud Zubeiry (bongostaz blog)
JAMAL Emil Malinzi, usiku huu ameshinda Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kupata kura 72, dhidi ya 52 za mpinzani wake Athumani Jumanne Nyamlani.
Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam, Walace Karia alifanikiwa kushinda nafasi ya Makamu wa Rais kwa kupata kura 67 akiwashinda Nassib Ramadhani kura 52 na Imani Madega sita.   
Huyu ndiye Rais wenu mpya TFF; Rais aliyemaliza muda wake TFF, Leodegar Tenga kushoto akimtambulisha Jamal Malinzi kuliakuwa Rais mpya wa shirikisho hilo usiku nwa kuamkia leo ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam 

Katika nafasi za Ujumbe; Kanda ya 13; kiungo wa zamani wa Simba SC Wilfred Kidau amepata kura 60 na kuwashinda Muhsin Said kura 50, Omar Abdulkadir kura 10 na Alex Kabuzelia kura nne.
Kanda 12; Khalid Mohamed Abdallah amepata kura 69 na kumshinda Davisa Mosha aliyepata kura 54.
Kanda ya 11 Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amepata kura 78 na kuwashinda Riziki Majala kura tano, Twahir Njoki kura mbili, Juma Pinto kura 26 na Farid Mbaraka kura 14, Kanda ya 10 ameshinda Hussein Mwamba aliyepata kura 63, huku Charles Komba akipata nne na Stewart Nasima 58.
Kanda ya tisa Othman Kambi aliyepata kura 84 yeye amewashinda Francis Bulame kura 30, wakati James 
Tenga akimkabidhi mpira Malinzi kuashiria yeye ndiye kiongozi mpya mkuu wa soka nchini

Anampa shada la maua ishara ya kumuachia madaraka

Kwaherini; Tenga akiwaaga Wajumbe
Mhagama aliyepata 93 amemshinda Zafarani Damoda aliyepata kura 11 na Kanda ya nane, Ngube Kiondo amepata kura 73 amemshinda Ayoub Nyaulingo kura 52.
Kanda ya Tano, Ahmed Iddi Mgoyi aliyepata kura 92 amemshinda Yussuf Kitumbo aliyepata kura 34, wakati Kanda Omar Walii Ali amepata kura 53 dhidi ya 19 za Ally Mtumwa. 
Anamkabidhi Katiba ya TFF

Anapongezwa na Mwenyekiti wa Azam FC, Sheikh Said Muhammad Said Abeid

Eley Mbise amepata kura  51 dhidi ya 53 kura 57 za Lamanda Swai. 
Mbasha Matutu aliyepata kura 63, amembwaga Vesastis Ligano aliyepata kura 61, wakati Vedastus Lufano aliyepata kura 51, amewashinda Jumbe Odesa Magati kura 11, Mugisha Galibona kura 24 na Samuel Nyalla kura 39 na Kanda namba moja, Karilo Samson hakuwa na mpizani akapita moja kwa moja.
Kamati mpya ya Utendaji TFF

Wadau Musley Ruwey kushoto na Said Tuliy kulia walikuwepo hadi mwishoNdugu waandishi nagombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji katikauchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kanda ya Pwani na Morogoro na nimeamua kugombea nafasi hiyo ili  kuleta mabadiliko ya kweli na kuleta fikra endelevu.
Naamini kabisa nikichaguliwa katika nafasi hiyo kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tutaleta mafanikio zaidi na hususani kupokea kijiti kwa viongozi wenzetu waliotangulia ambao wameweka mfumo mzuri wa utawala bora ndani ya shirikisho.
Ili mafanikio yaweze kupatikane ni lazima tuweke mpango endelevu kwa kuwekeza zaidi katika soka la vijana, kuandaa kozi ,warsha na makongamano yatakayotupa dira nzuri ya kukuza na kuwaendeleza vijana na mchezo wenyewe wa soka.
Kikubwa ambacho nitahakikisha ntalisimia kidedea ni kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi, kuandaa makocha, waamuzi chipukizi na upatikanaji wa vifaa vya michezo ikiwemo kuhakikisha viwanja vya michezo havitumiki kwa matumizi mengine na hivi vilivyopo viweze kuboreshwa zaidi.
Lingine ni kuhakikisha mikoa yote nchini inapata haki sawa katika kugawiwa rasilimali zinazopatikana kutoka kwa wadhamini na Shirikisho la kandanda duniani (FIFA) na kuhakikisha mfumo wa kutumia tiketi za elektroniki unaanza kutumika mara moja.
Mfumo huo utasaidia kumaliza tuhuma za ubadhirifu wa mapato ya milangoni katika mechi mbalimbali zinazofanyika nchini katika viwanja mbalimbali.Zinapopatikana pesa kwa wingi ndio tutakapoweza kutumia fursa hiyo kufanya maendeleo ya mpira wa miguu. 
Nafahamu majukumu mazito ambayo yanatakiwa kutekelezwa na kamati ya utendaji na nikiwa kama mjumbe nafahamu nchi yetu ambayo imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali katika uendelezaji wa michezo hasa mchezo wa soka. 
Kwa miaka 13 iliyokaa Uingereza niliweza kupata nafasi ya kufanya kazi  (Part time) pale BBC Swahili kwa kweli niliweza kupata ufahamu  wa hali ya juu sana kuhusu mpira wa miguu na kufanya utafiti wa kina katika michezo ikiwa ni pamoja na wachezaji wake, viwanja, kanuni na mbinu mbalimbali. 
Lakini mwaka 1999 niliweza kupata semina ya siku 45 nchini Brazili juu ya uongozi wa mpira wa miguu (Football Administration), hatua ambayo ilinipata weledi mkubwa  sana katika uongozi wa mchezo wa mpira wa miguu.
Nina uhakika kwa hayo yote niliyoyapata kabla na baada ya kuondoka nchini, yameweza kunipa mwanga sahihi wapi tunapotakiwa kwenda, lakini pia kupata fursa ya kuweza kutumia uzoefu wangu na hiki nilichokipata kuweza kutumia ndani ya TFF.
Hivyo nimeamua kuingia TFF ili kutumia uzoefu wangu katika kuleta mabadiliko ya kweli, pamoja na kuwa mchezaji wa timu ya Pan African mwaka 1993, pia na mchezaji wa timu ya Taifa ya Vijana mwaka 1994.
Lakini kwa hivi sasa ni mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama Cha soka mkoa wa Pwani, Mjumbe wa kamati ya masoko ya TFF na Mwenyekiti wa Chaa Cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA).
Juma Pinto

25th October 2013

Na Dina Ismail, Tanzania Daima
KILIO cha wadau wa soka ni kushuka kwa kiwango cha soka cha Tanzania kunakotokana na kufanya vibaya kwa timu ya taifa, Taifa Stars katika kampeni za kucheza fainali za Afrika na Kombe la Dunia. 
Stars chini ya kocha Kim Poulsen iliyokuwa  ikipigania tiketi ya fainali za Kombe la Dunia za mwakani nchini Brazil, imeishia njiani. 
Ikiwa katika Kundi C, Stars imemaliza kampeni Septemba 7 ikiwa nafasi ya tatu baada ya kuambulia pointi sita katika mechi sita ilizocheza dhidi ya Ivory Coast iliyomaliza kinara, Morocco na Gambia. 
Wakati Stars ikiambulia pointi sita, Ivory Coast imemaliza na pointi 14 ikifuatiwa na Morocco pointi tisa huku Gambia ikimaliza ya mwisho baada ya kujitwalia pointi nne.

SAFARI YA STARS BRAZIL: 
Stars ilianza kampeni ya Brazil kwa kucheza na Chad katika mtoano wa kuwania kuingia hatua ya makundi. 
Ilianza kuwafuata Chad nyumbani kwao N’Djamena Novemba 11, 2011 ambako walishinda 2-1, na waliporudiana Uwanja wa Taifa, Dar ves Salaam Novemba 15 mwaka huo walifungwa 1-0, lakini wakasonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2. 
Matokeo hayo yakaifanya Stars kuingia kwenye kampeni hizo rasmi za kwenda Brazi ikipangwa kundi C, na timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia. 
Stars ilianza kampeni yake Juni 2, 2012 kwa kuifuata Ivory Coast mjini Abidjan na kufungwa mabao 2-0, kisha Juni 10, 2012 ikarejea Uwanja wa Taifa kuisubiri Gambia na kuifunga mabao 2-1. 
Machi 24, 2013, ikawakaribisha Morocco kwenye Uwanja wa Taifa, na kushinda 3-1. 
Hata hivyo, Morocco wakiikaribisha Stars mjini Marrakesh Juni 8, 2013, waliutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kwa ushindi wa mabao 2-1. 
Wakitoka kufungwa na Morocco, Stars walirejea nchini kujiandaa kuwakabili Ivory Coast na kuchapwa 4-2. 
Kipigo kutoka kwa Ivory Coast, ndicho kilizima ndoto ya Stars kuingia hatua ya mwisho ya timu 10 bora kuwania nafasi tano za kwenda Brazil kwa bara la Afrika. 
Hiyo ni baada ya kipigo cha Stars kuiwezesha Ivory Coast  kufikisha pointi 13 ambazo zisingefikiwa na nyingine kwenye kundi hilo, hivyo mechi za mwisho kuwa za kusaka heshima tu kwa Morocco, Tanzania na Gambia. 
Septemba 7, Stars wakicheza mechi ya kukamilisha ratiba dhidi ya Gambia, walifungwa mabao 2-0, mjini Bakau, matokeo ambayo kwa kiasi kikubwa yamewavunja moyo Watanzania. 
Wengi wao wanajiuliza tatizo hasa ni nini kwa timu hiyo? Ni udhaifu wa benchi la ufundi chini ya Poulsen? Ni aina ya wachezaji waliomo kwenye kikosi hicho au kukosa maandalizi bora yanayohitajika kulingana na ugumu na uzito wa kampeni hizo? 
Kufanya huko vibaya, Stars imezidi kuporomoka kwenye viwango vya soka duniani. Sasa inashika nafasi ya 127, licha ya kuwahi kupanda hadi  nafasi ya 89, mwaka 2007.

VIWANGO: 
Nafasi ya Tanzania kwa ubora wa soka katika miaka mingine ni kama ifuatavyo: 2012 (130), 2011 (137), 2010 (116), 2009 (106),  2008 (99),  2007 (89), 2006 (110), 2005 (165), 2004 (172), 2003 (159) na 2002 (153). 
Mwaka 2001 (149), 2000 (140), 1999 (128), 1998 (118), 1997 (96), 1996 (89), 1995 (70), 1994 (74) na 1993 Tanzania ilishika nafasi ya 98. 
Ndani ya 2013, kiwango cha Stars kimekuwa kibadilika kama rangi za kinyonga, Januari nafasi ya 124, Februari (127), Machi (119), April (116), Mei (116), Juni (109), Julai (121), Agosti 128 na Septemba (128). 
Matokeo ya uwanjani na mwenendo wa Stars katika viwango vya soka ulimwenguni, vimekuwa ni kinyume na matarajio ya wapenzi na wadau wa soka nchini.

UDHAMINI: 
Kabla ya mwaka 2006, moja ya sababu za kufanya vibaya kwa Stars katika medani ya kimataifa kwa maana ya kampeni za Kombe la Mataifa Afrika na Kombe la Dunia, ni maandalizi duni kiasi cha kushindwa kuhimili kishindo. 
Fikra za wengi zikajielekeza kuwa pamoja na changamoto nyingine kama kutokuwepo kwa mfumo bora wa ukuzaji wa vipaji vya vijana, udhamini kwa Stars ulionekana kama ungeiwezesha timu hiyo kufanya vizuri. 
Ilitazamiwa iwe hivyo kwa vile wakati timu hiyo ikicheza bila udhamini, wachezaji walikuwa wakikusanywa na kufanya mazoezi ya pamoja kwa siku chache tu kabla ya mechi ya kimataifa kwa lengo la kukwepa gharama. 
Mazingira ya wakati huo yalikuwa magumu sana kiasi cha mchezaji kuona kuitwa Stars kama adhabu, hivyo kutoa visingizio kadha wa kadha vya kukwepa kujiunga na timu hiyo na walioripoti, hawakucheza kwa ari. 
Nani asiyekumbuka baadhi ya wachezaji hasa wa timu kubwa za Simba, Yanga na Mtibwa Sugar wakati huo, waliposingizia hili na lile ikiwemo ugonjwa au kuumia ikiwemo kujifunga bandeji ili kukwepa kuitwa Stars? 
Lakini, kuanzia mwaka 2006 chini ya utawala serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, hamasa ya kiongozi huyo katika maendeleo ya michezo ikaonekana kwa kuamua kumleta na kumlipa Kocha wa Stars, Mbrazil Marcio Maximo. 
Mbali ya Maximo, pia Stars ikapata udhamini mnono wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) pamoja na Benki ya NMB, hivyo wachezaji na viongozi wa timu hiyo kuanza kufurahia uwepo wao katika timu hiyo. 
Ikiwa chini ya udhamini huo, Stars ikaingia katika vita ya kupigania tiketi ya fainali za Afrika za mwaka 2008 nchini Ghana, ikipangwa kundi la saba, ilimaliza kampeni nafasi ya tatu ikivuna pointi nane, nyuma ya Senegal (11) na Msumbiji (9) huku Burkina Faso ikiburuza mkia kwa pointi nne. 
Kwa kushindwa kwenda Ghana, Stars ikaelekeza nguvu katika mbio za kucheza fainali za Afrika kwa nyota wa Ligi za Ndani (CHAN), ambazo kwa mara ya kwanza zilichezwa nchini Ivory Coast. 
Stars chini ya Maximo, ikawa miongoni mwa miamba nane iliyocheza michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huo kuanzia Februari 22 hadi Machi 8. 
Katika kundi lake la A, Stars ilimaliza nafasi ya tatu ikijikusanyia pointi nne nyuma ya Zambia (5) na Senegal (5) huku wenyeji Ivory Coast wakiwa nafasi ya nne kwa pointi 1. 
Katika kundi B, Ghana ilimaliza kinara kwa pointi tano ikifuatiwa na DR  Congo (4), Zimbabwe (3) na Libya. DR Congo ilifanikiwa kubeba ubingwa. 
Stars kwa mara nyingine ikiwa chini ya Maximo, ikashiriki kampeni ya kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini na Kombe la Mataifa Afrika nchini Angola mwaka 2010. 
Ikipangwa katika kundi la D, Stars ilimaliza nafasi ya nne ikiwa ya mwisho kwa pointi 5, ikitanguliwa na Morocco (11), Afrika ya Kati na Algeria (8).

STARS BAADA YA MAXIMO: 
Stars ikaingia katika kampeni ya kucheza fainali za Afrika mwaka 2012, nchini Gabon na Guinea ya Ikweta, ikiangukia kundi D, ambako ilimaliza ya mwisho kwa pointi tano ikitanguliwa na kinara Morocco (11), Afrika ya Kati (8) na Algeria (5). 
Kwa kuepuka fainali za Afrika kugongana na Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil, fainali hizo zikapangwa kuchezwa mapema mwaka huu nchini  Afrika Kusini huku Stars ilikosa tena tiketi chini ya Kocha Kim Poulsen.

NINI TATIZO? 
Msingi wa swali hili ni mazingira halisi ya sasa ya Stars kuwa tofauti na ilivyokuwa zamani (kabla ya 2006), kutokana na uwepo wa wadhamini kuanzia SBL na NMB hadi Kampuni ya Bia Tanzania (TBL). 
Baada ya kwisha kwa mkataba wa SBL na NMB, kuanzia Mei 9, mwaka 2012, Stars imekuwa chini ya TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager kwa udhamini wenye thamani ya shilingi bil 23 kwa miaka mitano. 
Ikiwa ni mwaka na miezi kadhaa, matunda ya udhamini huo ni makubwa kutokana na maandalizi na matunzo bora tenha ya uhakika kwa timu hiyo wakati wa kujiandaa na mechi ya kimataifa iwe ya ushindani au ya kirafiki. 
Mbali ya matunzo hayo, Stars wamepewa basi jipya lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 250, suti ya kisasa kwa kila mchezaji na kiongozi huku wasifu wa nyota tisa ukihifadhiwa kwenye DVD. 
Aidha, chini ya udhamini huo mnono, posho za wachezaji na viongozi sio tu zinalipwa kwa wakati, pia zimepanda kwa ujumla wachezaji wana uhakika wa yenye hadhi kiasi cha kila mchezaji kuona fahari kuitwa Stars. 
Vyote hivyo vimeongeza hadhi na thamani ya timu  hiyo kuanzia benchi la ufundi chini ya Kim, madaktari hadi wahudumu wa timu hiyo. 
Kwa wachezaji, mazingira bora yanawafanya kila mmoja wakiwmo chipukizi kutamani kuitwa kutimiza ndoto yao ya kutoa mchango wao kwa timu hiyo. 
Lakini, uwekezaji huo uliofanywa tangu, timu hiyo haijawa na uhakika wa kupata matokeo mazuri kiasi cha kucheza fainali za Kombe la Dunia wala zile za Afrika ambazo mara ya kwanza na mwisho ni mwaka 1980.

KAULI YA WADHAMINI

Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe anasema pamoja na kusuasua kwa timu hiyo katika medani ya kimataifa, wanajua mafanikio ya soka hayawezi kuja haraka kama wengi wangetamani iwe. 
Kavishe anasema wao wadhamini bado wana nia njema ya kuendelea kuidhamini Stars na kwamba ni matarajio yao timu itaendelea kuimarika siku hadi siku. 
Anasema jambo linalotia moyo zaidi wadhamini ni kuona wananchi bado wakiendelea kuisapoti timu yao wakionyesha imani kubwa, hivyo ni imani yao kuwa mafanikio yatapatikana tu. 
“Lengo hasa la mdhamini kwa sasa ni kuhakikisha Stars inafanikiwa kucheza  fainali za Kombe la Afrika za mwaka 2015,” anasema na kuwasihi Watanzania wasikatishwe tamaa na kushindwa kwenda Brazil. 
“Watanzania wasikate tamaa kwani mpira wa Tanzania ulikuwa bado, ni lazima kwenda hatu akwa hatua kama jinsi alivyoanza Kocha Kim Poulsen,” anasema Kavishe. 
Anasema wao wakiwa wadhamini wa timu hiyo, wanafarajika na mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika katika Stars tangu waanze kuidhamini Mei 9, 2012.

WADAU: 
Baadhi ya wadau wametoa mawazo yao akiwemo nahodha wa zamani wa Stars na Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime anasema tatizo kubwa la wachezaji wa Stars ni kutojitambua, hivyo kutojua dhamana yao. 
“Tuwe wakweli, yaonyesha wachezaji wetu hawajitambui, wao ndio wanacheza soka uwanjani, hivyo wanapokuwa dimbani wanapaswa kupigania ushindi kwa nguvu na akili zote,” anasema Maxime aliyekuwa nahodha wa timu hiyo wakati wa Maximo na kuongeza: 
“Wakati wetu, tulikuwa tukiingia uwanjani tunajua nini tunatakiwa kufanya kwa mashabiki na nchi yetu, kwa sababu tunakuwa tumebeba dhamana ya Watanzania wote, tulihakikisha tunapambana, japo kufungwa ni sehemu ya mchezo.” 
Kuhusu benchi la ufundi chini ya Kim, Maxime anasema haoni tatizo na kamwe halipaswi kulaumiwa limekuwa likitimiza wajibu wake katika kuwaelekeza wachezaji wacheze vipi, hivyo wa kulaumiwa ni wachezaji. 
Mtazamo wa Maxime ni kama wa beki wa zamani wa Simba na Stars, Boniface Pawasa akisema tatizo kubwa ni wachezaji kukosa wivu na kiu ya kweli ya ushindi na mafanikio, hivyo wengi wao kucheza kwa kutimiza wajibu, hivyo timu ishinde, ifungwe au sare yote kwao ni sawa tu. 
Anasema chini ya mazingira hayo, ndio maana timu imekuwa kama homa ya vipindi, leo inacheza vizuri na kupata ushindi na kesho inacheza hovyo, hivyo hata ushindi wake huonekana kama ni kutokana na udhaifu wa timu pinzani. 
“Wachezaji wanapaswa kuwa na wivu na kiu ya ushindi vinavyobebwa na uzalendo katika kupigania ushindi uwanjani kwa kutambua kuwa watanzania wanataka ushindi kutoka kwao,” anasema Pawassa. 
Hata hivyo, Pawassa anasema kwa vile kuna uhusiano mkubwa kati ya Ligi Kuu na Stars, kuna haja ligi ikaboreshwa zaidi ili iweze kutoa nyota bora wa timu ya taifa. 
Pawassa anasema kinyume cha hapo, Stars itaendelea kufanya vibaya licha ya kuwepo kwa udhamini mnono zaidi katika historia ya soka chini ya uwekezaji mkubwa wa kampuni ya TBL. 
Anashauri uwekezaji uliofanywa kwa Stars, ufanyike pia kwa klabu za Ligi Kuu wanakotoka wachezaji wa kuunda timu hiyo kwani ligi mbovu pia hutoa wachezaji wabovu. 
Naye Steven Mapunda ‘Garrincha’ aliyewahi kuchezea Majimaji ya Songea, Simba na Stars, anasema kufanya vibaya kwa Stars kunatokana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kushindwa kutoka ofisini na kwenda kufanya mipango na fitna za ushindi. 
Garrincha anatoa mfano wa enzi ya Maximo, timu ilikuwa ikifanya vizuri kiasi kutokana na baadhi ya viongozi kuwa na mbinu mbalimbali ikiwemo ya nje ya uwanja kuiwezesha Stars kupata ushindi. 
“Viongozi wa TFF waache kukaa ofisini huko kazi yake ni kuandika taarifa na mambo mengine, soka ni mipango kwani kwa kushindwa kufanya hivyo, hata wachezaji wanajiona kama yatima tu hivyo wanacheza kwa kutimiza wajibu,” anasema na kuongeza: 
“Inasikitisha sana kwa timu yetu kufungwa hata na Uganda ambao hawana kikosi bora kama chetu….lakini wanatufunga tena tukiwa nyumbani, hii kwa kweli inatuumiza sana wadau wa soka.” 
Garrincha anakwenda mbali na kusema kama TFF wameshindwa kuisimamia, wangeikabidhi kwa viongozi wa Simba au Yanga waone itakuwa vipi kwa maslahi ya timu hiyo.

KIM POULSEN: 
Akizungumza baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa jijini Dar es Salaam (DIA) wakitokea nchini Gambia kucheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi na kuchapwa mabao 2-0, Kim alieleza mengi. 
Akiwa na wachezaji 18 waliokuwa kwenye msafara wa timu hiyo ambayo ilirejea nchini Septemba 9 (siku mbili baada ya mechi), Kim alisema moja ya sababu ya kufungwa, ni kuwakosa nyota wake muhimu wapatao tisa kutokana na kutoruhusiwa na klabu zao na wengine kuwa majeruhi. 
Poulsen anasema kutokana na hali halisi ya kikosi, alilazimika kupanga vijana wasio na uzoefu wa kutosha kuziba pengo la wazoefu kama Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu na wengine waliokosekana. 
“Tumesikitishwa na matokeo, lakini kama nilivyosema Gambia waliita wachezaji wao wote wanaocheza nje, sisi tulikosa karibia kikosi kizima cha kwanza...vijana waliocheza walijitahidi, lakini wenzetu waliwazidi uzoefu,” anasema. 
Anasema ni muhimu watanzania watambue kuwa mechi za kufuzu kucheza kombe la dunia zimekuwa muhimu sana kwa Tanzania kwani wachezaji wengi wametambulika na wameitwa nje. 
“Kuna wachezaji kama Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto ambao kutokana na mechi hizi wamepata nafasi ya kwenda kucheza nje,” anasema. 
Kocha huyo anasema yuko makini sana kutekeleza mpango wa muda mrefu ambao ni kuhakikisha Tanzania inafuzu kucheza Kombe la Afrika 2015 na kuongeza kuwa timu anayoendelea kujenga itafanya kazi hiyo. 
Anasisitiza kuwa ni lazima TFF ihakikishe wachezaji wote muhimu wanakuwepo wakati mechi za kufuzu kucheza Kombe la Afrika zitakapoanza mwakani. 
“Kwa sasa wachezaji watarudi vilabuni kwao na baada ya muda mfupinitawaita tena ili tujiandae na michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), yatakayofanyika Nairobi,” anasema.
Hata hivyo, anawasihi Watanzania wawe na subira kwani ana imani na timu anayoijenga.
“Tungefurahi kama tungefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia, lakini ni mapema sana kwa timu yetu ambayo bado inajengwa…tumpe kocha nafasi aweze kutimiza haya malengo na sio kumkatisha tama,” anasema.

0788344566 dinazubeiry@gmail.com
Uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League- TPL Board) unafanyika kesho (Oktoba 25 mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower kuanzia saa 3 asubuhi. 
Mgeni rasmi katika mkutano huo wa Bodi ya TPL ambao unafanyika kwa mara ya kwanza atakuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga. 
Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL). 
Viongozi wa klabu za FDL wamefikia hoteli ya Royal Valentino iliyoko Barabara ya Uhuru wakati wale wa VPL ambao pia watashiriki Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wamefikia hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo. 
Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inawasili nchini kesho (Ijumaa, Oktoba 25 mwaka huu) saa 8.30 mchana tayari kwa mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania itakayofanyika Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu). 
Msumbiji itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ndege ya LAM ikiwa na msafara wa watu 25 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi. Timu hiyo itafikia kwenye hoteli ya Sapphire iliyopo maeneo ya Gerezani, Dar es Salaam. 
Mara baada ya kuwasili JNIA, kocha na nahodha wa timu hiyo watazungumza na waandishi wa habari juu ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. 
Kwa upande wa U20 chini ya Kocha Rogasian Kaijage imejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo, na kesho saa 10 jioni itafanya mazoezi yake ya mwisho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Viingilio kwa mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na rangi ya chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 10,000. 
Kamishna wa mechi hiyo Evelyn Awuor kutoka Kenya tayari amewasili nchini wakati waamuzi kutoka Burundi wanatarajia kuwasili leo saa 1 usiku kwa ndege ya Kenya Airways wakiunganishia safari yao Nairobi, Kenya. Maofisa wote wa mechi hiyo wanafikia hoteli ya New Africa.

RAGE

CHANZO:Liwazozito blog
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema atawachukulia hatua za kinidhamu, viongozi watakaobainika kuingililia kazi na majukumu ya benchi la ufundi la timu hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Tabora jana, Rage alisema hakuna kiongozi anayeruhusiwa kumpangia timu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdalla Kibadeni.
Rage ametoa tishio hilo baada ya Kibadeni kukaririwa wiki hii akisema kuwa, baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wamekuwa wakimshinikiza kuwachezesha wachezaji wanaowapenda.
Kwa mujibu wa Kibadeni, viongozi hao walitaka kuingilia majukumu yake kabla ya mchezo wao wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba, uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
"Kibaden ni kocha halali wa Simba,ana mkataba na amesomea fani hiyo, hivyo kama kuna kiongozi ameingilia kati majukumu yake, tutamshughulikia,"alionya Rage.
Wachezaji, ambao Kibadeni amelalamika kwamba, amekuwa akishinikizwa kuwachezesha ni pamoja na kiungo, Abdulharim Humud, ambaye alionyesha kiwango cha chini katika mechi dhidi ya Yanga.
Katika mechi hiyo, Simba na Yanga zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 3-3. Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 3-0 baada ya dakika 45 za kwanza, lakini Simba ilizinduka kipindi cha pili na kusawazisha.

IMANI OMARI MADEGA

Na Deodatus Mkuchu, gazeti la Tanzania Daima
UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), umepangwa kufanyika Oktoba 27, ukitanguliwa na ule wa Bodi ya Ligi Kuu ambao utafanyika siku mbili kabla; yaani Oktoba 25.
Ni uchaguzi utakaohitimisha utawala wa Rais Leodegar Chilla Tenga aliyeingia madarakani mara ya kwanza Desemba 27, 2004 kabla ya kutetea kiti hicho uchaguzi uliofuata wa Desemba 14, 2008.
Miongoni mwa wagombea wa nafasi ya Makamu wa Rais, ni Imani Mahugila Madega, atakayechuana na Ramadhan Nassib aliyewahi kuwa Makamu wa Pili wa Shirikisho hilo akiwakilisha Klabu za Ligi Kuu na Wallace Karia, Mwenyekiti wa Kamati Mpito ya Ligi.
Katika mahojiano yake na Tanzania Daima, Madega anasema amejitosa kwenye nafasi hiyo ili kutumia elimu, vipaji alivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu na uzoefu kusaidia harakati za kuendeleza mchezo huo.
Madega, mwanasheria kitaaluma, anasema kwa vile amekuwa na uzoefu wa kutosha wa kuongoza soka kuanzia ngazi ya klabu, mkoa hadi taifa, haendi TFF kujaribu kuongoza bali akiwa na uhakika wa nini anakwenda kufanya.
“Nina kiu ya kuleta mageuzi zaidi ya soka kwani kwa kipindi cha zaidi ya miaka nane ambayo nimekuwa kwenye uongozi kuanzia ngazi ya klabu, mkoa hadi taifa, nimejifunza mengi, hivyo nagombea nikijua nakwenda kufanya nini kama nitachaguliwa,” anasema.
Madega anasema akiwa mwenyekiti wa Yanga (2007-2010), alijifunza mengi hivyo anajua klabu zinahitaji nini ziweze kupiga hatua zaidi kisoka na kiuchumi kwa maslahi ya vijana.
Anasema kwa vile michezo sasa si afya na burudani tu kama ilivyokuwa zamani hasa kutokana na kuwa ajira kwa wenye vipaji na taaluma mbalimbali, kumbe ni sekta inayohiji uwekezaji wa nguvu.
Madega anasema kwa miaka minne aliyokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF 2004 -2008 na baadaye kuwa mjumbe wa Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji kwa miaka minne 2008 hadi 2013, anayajua mengi.
“Naamini kupitia taaluma yangu ya sheria, uzoefu wangu wa kuongoza kuanzia ngazi ya klabu, mkoa hadi taifa na kukulia mazingira ya soka tangu nikiwa shuleni, najua vitakuwa chachu ya mafanikio,” anasema.
Anaongeza, kwa vyote hivyo alivyojaaliwa kuwa navyo, anajiona mwenye deni kwa taifa lake, hivyo namna pekee ya kulipa ni kuitumikia soka akiwa Makamu wa Rais wa TFF.
Anasema pamoja na kutambua weledi wa wajumbe wa mkutano mkuu katika kufanya maamuzi kwa maslahi ya soka la Tanzania, bado anawakumbusha kuwa wasifanye makosa ambayo yataligharimu soka kwa miaka minne.
“Nawasihi na kuwaomba wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba wana deni kubwa kwa Watanzania, hivyo wanapaswa kufanya maamuzi yatakayoleta mageuzi ya mchezo huo kwa kuchagua viongozi wenye uwezo na waadilifu.”
Anasema hatakuwa sahihi akisema uongozi wa Rais Leodegar Chilla Tenga haujafanya kitu kwa sababu umefanya mengi hasa kujenga misingi imara ya utawala wa mchezo huo kiasi kwamba imekuwa taasisi kamili.
Madega anasema pamoja na mafanikio hayo chini ya mgawanyo wa majukumu kupitia idara mbalimbali, pia yapo mengi yanayohitaji kufanyiwa kazi zaidi na viongozi wajao.
Anasema msingi bora uliojengwa chini ya utawala wa Tenga, umeifanya TFF kuaminika mbele ya wadau na jamii na kusema kama atashinda, kazi mojawapo ni kuyaenzi kisha kupiga hatua mbele zaidi hasa uwekezaji.
Madega anasema uwekezaji ambao kama atashinda ataupigania zaidi ni soka ya vijana akiamini ndio msingi wa mafanikio ya mchezo huo duniani kote.
Jambo jingine ambalo atalisimamia ni soka ya wanawake ambayo licha ya uwepo wa vipaji vingi kila kona nchini, hakuna ligi wala mashindano ambayo vijana wataonyesha uwezo wao ili kutwaliwa na timu mbalimbali.
Uwazi
Madega anasema chini ya Tenga, TFF imejitahidi kujenga uaminifu mbele ya jamii na ndio maana leo hii soka imekuwa na wadhamini mbalimbali kama Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Kilimanjaro Premium Lager na Coca Cola inayodhamini michuano ya vijana wa chini ya miaka 15.
Aidha, kuna wadhamini wa Ligi Kuu, kampuni ya Vodacom na wengineo wadogo kama Uhai kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vijana wa chini ya miaka 20, lakini bado juhudi zinatakiwa za kuwapata wadhamini zaidi katika mchezo huo.
“Kazi ya TFF si kuuza soda, bali kuendeleza soka, hivyo pamoja na juhudi kubwa iliyofanywa na Tenga, soka haijawa na heshima yake kwa asilimia 100 kwa sababu yapo makosa yalifanyika,” anasema.
Madega anasema, baada ya Tenga kujenga msingi, kazi iliyobaki ni soka kuchezwa kwa maana ya kuwa na mfumo bora zaidi wa ligi kuwezesha mchezo huo kuchezwa mikoa yote.
Anasema kitendo cha soka kuonekana kuchezwa au kunawiri kwa baadhi tu ya mikoa, si kitu kizuri kama kweli tunataka mchezo huo ufike kwenye mafanikio makubwa kwa maslahi ya vijana na taifa kwa ujumla.
Soka ya vijana/ wanawake
Madega anasema kwa kutambua nini msingi wa mafanikio ya soka kote ulimwenguni, kama atachaguliwa kwenye nafasi ya Makamu Rais, atajitahidi kupigania soka ya vijana sio tu uwepo wa vituo hai vya kukuza vipaji vya watoto, pia kuboresha mashindano mashuleni.
Anasema ufumbuzi wa soka la Tanzania ni kurejesha mfumo wa zamani wa mashindano mashuleni kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuo ambapo kijana alikuzwa kimchezo kutoka ngazi moja hadi nyingine.
Anaamini uwepo wa mashindano bora ya vijana mashuleni, utachangia kupatikana kwa vipaji vipya kila mwaka kama ilivyokuwa zamani ambapo nyota wengi walitokea kwenye mashuleni, Kombe la Taifa na timu za makampuni na mashirika.
Madega anasema uwepo wa mashindano katika shule, himizo la serikali kuwa michezo ni mahali popote pa kazi, michezo kwa ujumla wake ilishamiri kila kona ya nchi tena ikichezwa kulingana na umri.
Anasema ni kwa mfumo huo ndipo hata timu ya taifa itapata nyota bora wenye uwezo mkubwa kisoka kama ilivyokuwa zamani ambapo mchezaji aliyeitwa kikosi cha taifa, alikuwa na uwezo kamili kiuchezaji.
Ufundi
Madega anaamini ili soka iweze kupiga hatua kubwa mbele, pamoja na uwepo wa programu mbalimbali za vijana, soka ya wanawake na ile ya ufukweni, juhudi zifanyike katika uwekezaji kwenye masuala ya ufundi.
Anasema kama nchi itakuwa na makocha bora wa kutosha kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya hadi vitongoji, itasaidia kuibuliwa kwa vipaji vingi vya kufuata nyayo za kina Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Madega, mwenye uwezo na uzoefu mkubwa katika kuongoza soka akisaidiwa na taaluma ya sheria katika kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali za mchezo huo, anaamini tatizo la soka ya Tanzania sio uhaba wa vipaji, bali kukosekana kwa miundo mbinu bora na sahihi.
Madega anadokeza kuwa kwa kutambua kuwa nchi inakabiliwa na uhaba wa viwanja bora vya soka na TFF haina viwanja, akishinda atashawishi baadhi ya viwanja vikodiwe na shirikisho hilo.
“Japo najua kuna ushirikiano mzuri kati ya TFF na wamiliki, kama nitashinda nitajitahidi kushawishi kuangalia uwezekano wa shirikisho hilo kukodi viwanja hivyo ili kuviendesha na kuvisimamia vizuri,” anasema Madega.
Soka ya wanawake
Madega anasema kama ilivyo kwa wanaume, ndivyo ilivyo kwa wanawake kwani vipaji vimetapakaa kila kona ya nchi, tatizo ni kukosekana kwa mfumo bora wa kuviibua na kuviendeleza kwa maslahi yao na taifa.
Anasema kama kungekuwa na mfumo bora wa kuibua na kuendeleza vipaji vya soka ya wanawake, leo kocha wa timu ya taifa, Twiga Stars, Rogasian Kaijage, asingekuwa akiokoteza wachezaji kama anavyofanya.
“Jiulize Kaijage ni kocha wa Twiga Stars na soka ya wanawake kwa ujumla wake, anapata wapi vipaji wakati hakuna hata ligi ya soka ya wanawake?
“Vipi unawezaje kupata nyota wa kiwango cha kuchezea timu ya taifa bila kuwepo kwa mashindano? Sana sana atakachofanya kocha ni kuokoteza tu, jambo ambalo lina madhara kwa timu husika,” anasema.
Anasema tatizo hilo linaweza kupata ufumbuzi kwa kuboresha mashindano ya michezo mashuleni ikiwemo soka ya wanawake ili kupata vipaji vipya kila mwaka na kuviendeleza kwa kuwa na ligi ngazi ya wilaya hadi mkoa.
“Hili likifanyika kwa dhati, naamini soka ya wanawake itashamiri na kupata mafanikio makubwa yatakayoitangaza nchi kimataifa kwani mfumo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika na kimataifa, si mgumu kama ilivyo kwa wanaume,” anasema.
Madega anasema kama wajumbe wa Mkutano Mkuu watamchagua katika nafasi ya Makamu wa Rais, atashirikiana na wenzake kupigania mafanikio ya soka ya vijana na wanawake akitambua kuwa soka ni ajira kwa vijana.
Kutengeneza fedha
Anasema jambo jingine ambalo atalipigania kwa kushirikiana na wenzake kama atachaguliwa ni kuhakikisha TFF inakuwa na vyanzo mbadala nje ya mapato ya milangoni na udhamini au ufadhili.
“Tunajua soka haiwezi kwenda mbele bila udhamini, ufadhili na uungwaji mkono wa wadau, lakini nje ya hayo TFF ina vyanzo gani mbadala?
“Kama nikichaguliwa, kwa nafasi hiyo nitashawishi shirikisho liwe na vyanzo vingine nje ya viingilio na wadhamini ili kujenga uwezo mzuri kiuchumi kujiendesha.
Anasema kukosekana kwa vyanzo mbadala, ndio maana Twiga Stars na timu ya wanawake wa chini ya miaka 20 iliyo kambini kwa sasa, zimekuwa zikikabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha hadi kuhitaji misaada ya wadau.
Anasema hiyo ni tofauti na ilivyo kwa timu nyingine kama Stars iliyo chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premier Lager na mashindano ya vijana wa chini ya miaka 15 chini ya udhamini wa kampuni ya Coca Cola.
Madega anasema kama akichaguliwa atajitahidi kubuni vyanzo vipya ili kuwa na uwezo wa kuhudumia timu ambazo hazina udhamini wakati huohuo kuongeza juhudi za kusaka wadhamini wengi kadiri itakavyowezekana.
Akidokeza kuhusu miradi mbadala inayoweza kuwa chanzo cha fedha, Madega anasema ni mauzo ya jezi za timu ya taifa akiamini kama wapenzi na mashabiki watahamasishwa kwa njia mbalimbali na kufanya vizuri kwa timu husika, watanunua kwa wingi jezi za timu yao.
Anaongeza kuwa njia nyingine inayoweza kuwa chanzo cha mapato kwa TFF, ni suala la haki ya matangazo ya kurusha mechi za Stars katika televisheni mbalimbali.
Madega anaamini kama maeneo hayo mawili yatasimamiwa vizuri kwa maana ya uwajibikaji uliogubikwa na uadilifu, hata mapato yatokanayo na viingilio, yataonekana akiamini eneo hilo bado kuna matatizo.
Anasema kama TFF itajenga mazingira ya uwazi, uwajibikaji na uadilifu katika eneo hilo, ndipo chombo hicho kitazidi kuaminika mbele ya wadau na jamii, hivyo kuvutia wawekezaji zaidi katika mchezo huo.
Ushauri kwa serikali
Madega anasema kama atashinda, shirikisho hilo litaishauri serikali kupitia wizara husika kuangalia upya mahali tulipojikwaa kimichezo, ikiwezekana kuboresha zaidi mashindano mashuleni kuanzia msingi hadi sekondari.
Anakwenda zaidi ya hapo akisema, pamoja na uwepo wa mashindano katika ngazi hizo, bado hakujawa na mafanikio ya kuibuliwa kwa vipaji kama ilivyotarajiwa kutokana na changamoto mbalimbali hasa miundombinu.
Madega anasema ukifanya uchunguzi katika shule mbalimbali za msingi hadi sekondari, nyingi (hasa za mijini) hazina viwanja na vifaa vya michezo kama ilivyokuwa zamani.
“Tembelea shule za Dar es Salaam, uone kama zina viwanja…utakuta eneo ambalo lilikuwa wazi, limejengwa sekondari ya kata. Sasa jamani, hata hao watoto wanaoshiriki UMITASHUMTA na UMISSETA, wanajifunza wapi?
Anasema anavyojua, eneo la shule linapaswa kuwa si chini ya ekari 10, kwa maana ya eneo la madarasa, ofisi za waalimu, uwanja na eneo la matumizi mengine ya ardhi, lakini jambo hilo kwa sasa halipo tena.
Madega anasema kama atafanikiwa kushinda, ataketi na wenzake kwa maana ya Kamati ya Utendaji kuangalia nini wafanye akiamini yapo yanayoweza kufanywa na shirikisho hilo na mengine ni ya serikali.
Klabu
Madega anasema kama atachaguliwa, atatumia nafasi yake kuhimiza klabu kuwekeza kwenye soka ya vijana sio tu kuwa na timu ya vijana wa chini ya miaka 20, bali ikiwezekana kuanzia vijana wa kuanzia miaka sita hadi 12.
Anasema kwa vile amekuwa kiongozi wa klabu kwa miaka minne, anayajua vizuri matatizo yaliyopo katika ngazi hiyo, lakini ni jukumu la viongozi wa klabu kutambua soka ya vijana ndio siri ya mafanikio.
Udau wake katika soka
Anasema mbali ya kuipenda soka tangu akiwa mdogo na kuicheza katika ngazi ya shule ya msingi, sekondari hadi vyuoni, amekuwa kiongozi wa mchezo huo kwa muda mrefu na katika ngazi ya klabu, mkoa hadi taifa.
Mwaka 2000, alikuwa miongoni mwa maseneta wa klabu ya Yanga chini ya mfumo wa kampuni wakati huo Abbas Tarimba akiwa rais kabla ya kumwachia Francis Mponjoli Kifukwe.
Mwaka 2003, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (Corefa) na Desemba 27, 2004-2008, alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Leodegar Chilla Tenga.
Anasema akiwa TFF, kwa kutumia taaluma yake ya sheria alishiriki kikamilifu kuhakikisha shirikisho hilo linakuwa na katiba bora na kanuni zake ambazo kwa kiasi kikubwa zimeifanya soka iheshimike.
Mei 31, 2007, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga hadi Mwaka 2010, wakati huohuo akiwa mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF nafasi ambayo anayo hadi sasa.
Anasema ni kiongozi pekee aliyeondoka Yanga akijivunia kuacha kiasi cha sh mil. 209, jambo ambalo limewashinda wengi ndani na nje ya klabu hiyo.
Zaidi ya fedha, Madega anajivunia kuiachia klabu hiyo alama ya biashara ya klabu hiyo (trade mark) ambayo kama itatumiwa vizuri ni chanzo cha uhakika cha mapato kwa maendeleo ya klabu hiyo mkongwe.
Madega anasema vyote hivyo vinaakisi uadilifu wake katika utendaji wa majukumu yake akiamini cheo ni dhamana na mzigo mzito wa kuwatumikia watu katika kukidhi matarajio yao, yaani mafanikio ya soka.
Wito kwa wajumbe
Madega anasema kwa vile wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, wanajua kuwa wamebeba dhamana kubwa ya hatima ya soka la Tanzania, wafanye maamuzi yatakayoipeleka soka mbele zaidi sio kurudisha nyuma ya hapa ilipo.
“Dhamana ya soka la Tanzania iko mikononi mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
“Niseme hawa wamepata bahati kubwa ya kuibeba dhamana hiyo kwa niaba ya zaidi ya Watanzania milioni 45; Watanzania wasingependa kuona uchaguzi unatawaliwa na ushabiki,” anasema.
Madega anawasihi wajumbe wafanye maamuzi wakiongozwa na utashi wa maendeleo ya soka katika kuchagua watu wenye uwezo, weledi, uadilifu usiotiliwa shaka katika rekodi zao ili TFF ipate watu sahihi.
“Binafsi, nina imani kubwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu kwani kwa uchunguzi wangu, nimebaini ni waelewa wa mambo tena ni wenye heshima zao na elimu nzuri, hivyo wanajua wanachokifanya.