MISS TANZANIA ZAIDI YA SHINDANO, LIMEWATOA WENGI

Na Dina Ismail
MIAKA ya nyuma  shindano la Miss Tanzania lilikuwa likichukuliwa kama uhuni  kiasi cha wazazi kukataza watoto wao kushiriki.
Lakini kadiri miaka ilivyosonga ndipo wazazi walianza kulikubali shindano hilo kwa kuruhusu watoto wao baada ya kuona mafanikio waliyoyapata baadhi ya warembo mara baada ya kushiriki shindano hilo.
Miss Tanzania ‘beauty with purpose’ ni zaidi ya shindano kwani mrembo anaweza asishinde taji kuu lakini akanufaika kutokana na ushiriki wake.
Kwa mantiki hiyo kuna baadhi ya wadada ambao walipata kushiriki shindano hilo leo hii wamejijengea heshima kubwa katika jamii kutokana na kazi wanazozifanya, lakini heshima inaanzia kushiriki kwao Miss Tanzania.
Kihistoria shindano hilo kwa hapa nchini lilianza rasmi mwaka 1960 na mrembo wa kwanza kutwaa taji hilo alikuwa Theresia Shayo ambaye sasa hivi ni marehemu.
Hata hivyo kutokana na maadili na utamaduni wa Tanzania serikali ililifuta mwaka 1967 kabla ya kurejeshwa tena katika miaka ya 1990 na ndipo hapo Tanzania ilianza kupata mafanikio kupitia mashindano ya urembo.
Mrembo  Aina Maeda ndiye alikuwa mrembo wa kwanza tangu kurejeshwa kwa mashindano hayo ambapo alitwaa taji hilo mwaka 1994 yakiwa chini ya uratibu wa Hashim Lundenga.
Mashindano hayo yalianza kwa kuendeshwa kimkoa na kadiri miaka ilivyosogea wigo wake ulitanuka na kufikia kufanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara, wilaya, vitongoji  na hata katika ngazi ya vyuo vya elimu ya juu kulisakwa washiriki.
Kupitia mashindano hayo, pamoja na zawadi nono za nyumba, magari pamoja na mamilioni ya fedha, tumeshuhudia warembo mbalimbali wakijipatia umaarufu ambao uliwawezesha kupata kazi katika makampuni mbalimbali, mikataba katika makampuni mbalimbali ya matangazo na mengine mengi.
Hawa ni baadhi ya warembo waliopitia Miss Tanzania na sasa hivi wanaheshimika kutokana na kazi wanazozifanya sambamba na mchango wao mkubwa katika jamii:
Hoyce Temu:
Huyu ni Miss Tanzania mwaka 1999 ni mrembo ambaye amekuwa mfano wa kuigwa kwa  kufanya zaidi shughuli za kijamii   kwani tangu atwae taji hilo jina lake limebaki kuwa juu kila uchwao.
Mrembo huyo licha kipindi chake cha mwaka mmoja cha kufanya kazi za kusaidia jamii kama Miss Tanzania lakini ameendelea kuifanya hivyo hadi sasa  ambapo kupitia kipindi chake cha Televisheni cha ‘Mimi na Tanzania’ amekuwa akiongea na watu wenye shida mbalimbali na kuwaombea misaada kwa wasamaria.
Hoyce ambaye kwa sasa anafanya kazi kitengo cha mawasiliano na Mahusiano katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) nchini Kwa kutambua huduma yake kwa jamii, aliwahi kutajwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga kama mlimbwende bora kuliko wote.
Nancy Sumari:
Alitwaa taji la Miss Tanzania 2005, pia taji la Miss World Afrika mwaka huo.
Ni mrembo mwingine msomi na anayeheshimika hapa nchini kutokana na utumishi wake katika jamii.
Nancy ni mfanyabiashara, pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bongo Media, pamoja na Mfuko wa  The Neghesi Sumari Foundation.Pia ni mtunzi wa kitabu cha hadithi za watoto kiitwacho, Nyota Yako.
Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lyn’:
Ni mrembo aliyetwaa taji mwaka 2000.Kabla ya kushiriki shindano alikuwa akijihusisha na uimbaji wa muziki katika bendi ya Tanzanite.
Baada ya kumaliza kulitumikia taji lake aliendelea kuwa msanii ambako alitoa singo zake kama msanii wa kujitegemea huku vibao vyake kama Crazy Over You, Nipe mkono, Best na nyinginezo ambazo zilimpatia umaarufu zaidi.
K-Lyn ambaye ni mke wa mfanyabiasha maarufu nchini Reginald Mengi kwa sasa amejikita zaidi katika biashara akimiliki duka la liitwalo Amorette ambalo linatengeza na kuuza thamani za ndani pamoja na upambaji wa ndani.
Jokate Mwegelo:
Jina lake lilianza kusikika zaidi mwaka 2006 aliposhika nafasi ya pili katika shindano la Miss Tanzania, huku taji hilo likitwaliwa na Wema Sepetu.
Jokate alitwaa taji la balozi wa kinywaji cha Redd’s kilichokuwa mmoja ya wadhamini wa shindano hilo ambapo aliweza kufanya kazi mbalimbali zilizohusiana na mitindo na ubunifu kama balozi.
Baada ya muda wake kumalizika Jokate alionekana kupenda zaidi masuala ya mitindo ambapo alijikita katika sekta hiyo, sambamba na kujihusisha na uigizaji na muziki.
Kwa sasa Jokate amejikita zaidi katika biashara chini ya Lebo yake aliyoipa jina la Kidoti ambapo ameshaingiza sokoni bidhaa zake kadhaa ikiwemo nywele, mabegi ya shule na kandambili.
Aidha, mrebo huyo pia anaendesha kampeni yake iitwayo ‘Be Kidotified’ inayohamasisha wanafunzi wenye vipaji mbalimbali kutojiweka nyuma.

Happiness Magesse ‘Millen’:
Jina lake linang’ara duniani kwa sasa kupitia fani ya mitindo.
Alitwaa taji la Miss Tanzania mwaka 2001 na baada ya kumaliza muda wake alikwenda nchini Afrika Kusini na kuanza kujihusisha na kazi ya mitindo ambayo anaifanya mpaka sasa.
Millen ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani pia anamiliki mfuko wake uitwao ‘Millen Foundation’ ambao ni mahususi kwa kuendesha kampeni maalum ya kuelimisha wasichana juu ya ugonjwa wa Endomitriasis ambao huwasababishia maumivu makali wakati wa siku zao za hedhi.

Hao ni baadhi kwani wapo warembo wengi tu  waliopitia katika shindano hilo ambao wanafanya mambo makubwa ya kueleweka katika jamii.