SIMBA CHEZENI MPIRA ACHENI KULIALIA

Na Dina Ismail
SIMBA  imejikuta ikihaha kupigania mabao matatu na pointi tatu ilizopokwa na  kamati  ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Vinara hao wa ligi kuu walikata rufaa kwa kamati ya usimamizi na uendeshaji wa Ligi Tanzania ‘kamati ya masaa 72’ ikidai Kagera Sugar kumchezesha beki mohammed Fakhi  wa Kagera Sugar wakati akiwa ana kadi tatu za njano.
Katika mchezo huo uliopigwa katika dimba la Kaitaba mjini Bukoba  Aprili 2 mwaka huu, Simba ililala kwa mabao 2-1.
Kwamba, kamati ya masaa 72 iliipa mabao matatu na pointi tatu  Simba baada ya kujiridhisha kwamba  Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano.
Hata hivyo Kagera Sugar ilipinga na kukimbilia kamati ya katiba Sheria na Hadhi wachezaji  kabla ya kamati hiyo kuamua kuipoka ushindi huo wa mezani Simba baada ya kugundua kuwepo kwa makosa kadhaa katika kuipa ushindi wa mezani Simba.
Selestine Mwesigwa, Katibu Mkuu wa TFF akizungumzia hatua hiyo alibainisha mambo kadhaa yaliyopelekea kubatilishwa kwa maamuzi hayo ikiwemo Simba kutowasilisha kwa wakati na hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 20 kifungu cha kwanza cha kwanza cha kanuni za Ligi Kuu toleo la mwaka 2006 inayotaka malalamiko yote yawasilishwe kwa maandishi Bodi ya Ligi siyo zaidi ya saa 72 baada ya mchezo kumalizika kwa mchezo.
Pili, Mwesiga alisema  malalamiko hayo hayakulipiwa ada kwa mujibu wa kanuni ya 20 kifungu cha nne kinachosema ada ya malalamiko ni Sh. 300,000 na kwamba malalamiko yatakayowasilishwa bila kulipiwa ada au baada ya muda uliowekwa hayatasikilizwa.
Sababu ya tatu aliyoitaja Mwesigwa ni kwamba kikao cha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kilikosa uhalali baada ya kuwashirikisha Wajumbe waalikwa ambao siyo sehemu ya Kamati hiyo.
Maamuzi hayo yameonekana kuichanganya sana Simba na hivyo kuwa na mikakati ya kuhakikisha inapanda ngazi za juu zaidi ili kuweza kudai haki yao.
Nadhani Simba ingeachana na hili suala na kuelekeza nguvu zake katika michezo yake ya Luigi ambayo imebakiza wiki chache kabla ya kumalizika.
Kwamba, inawezekana ni kweli wana haki lakini walifanya makosa wenyewe katika hatua za awali za kukata kwao rufaa kwa kukosea baadhi ya kanuni na taratibu zilizopo katika katika ya TFF kama kama alivyoeleza Katibu Mkuu wa TFF
Hivyo basi kuendelea kufuatilia suala hilio ni kupoteza muda kwani nguvu inayotumika katika zoezi hilo ni bora ingeelekezwa katika maandalizi ya michezo iliyonayo timu hiyo ambayo kwa sasa inaongoza Ligi hiyo  ikiwa na pointi 59, huku mabingwa watetezi Yanga wakishika nafasi ya pili kwa pointi 56.

Sote tunafahamu Simba imepania kutwaa ubingwa wa Bara msimu wa 2016/2017 baada ya kuukosa kwa miaka zaidi ya mitano hivyo ni vema ikajiongeza kwa kupata ushindi wa halali badala ya kubaki inaililia pointi za bure.

Comments