SAPOTI KUBWA KWA TIMU YA TENISI KWENYE KOMBE LA DUNIA

Na Dina Ismail
KWA muda mrefu Tanzania tumekuwa wasindikizaji katika michezo mbalimbali na hasa katika ngazi ya kimataifa.
Licha ya kuwepo kwa wachezaji wengi wenye vipaji katika michezo husika lakini tumejikuta tukiishia njiani katika harakati za kusaka tiketi ya kucheza kombe la dunia.
Bahati nzuri tumekuwa tukipata nafasi za kushiriki katika kuwania kucheza mashindano mbalimbali ya dunia lakini tumekuwa tukiishia njiani tu na hata tukibahatisha tunatolewa mapema.
Hivi karibuni timu ya Taifa ya Tenisi kwa watu wenye ulemavu imeweza kuitoa kimasomamso Tanzania baada ya kufuzu kucheza  mashindano ya kombe la dunia kwa mchezo huo.
Timu hiyo ilifuzu hatua hiyo bada ya kushika nafasi ya kwanza  katika michuano ya Afrika iliyofanyika Nairobi, Kenya  na hivyo itaiwakilisha Afrika katika mashindano ya Dunia yatakayofanyika nchini Italia mwezi Mei mwaka huu.
Ni hatua kubwa na ya kupongezwa kwa timu hiyo pia ni  jambo la kujivunia  kwani  pamoja na kudaiwa kufanya maandalizi katika mazingira magumu lakini waliweza kukabiliana na changamoto walizokutana nazo na hatimaye waliweza kushinda.
Kocha wa timu hiyo, Riziki Salum alikaririwa na vyombo vya habari akizungumzia changamoto  mbalimbali walizokumbana nazo  katika mashindano hayo lakini hawakukata tamaa na kuhakikisha wanaitoa kimasomaso Tanzania na Afrika kwa jumla.
Riziki alieleza kwamba walikuwa wakifanya mazoezi na maandalizi yao katika mazingira magumu lakini wachezaji wake waliweza kukabiliana na hali hiyo na kufanya kile walichodhamiria na matokeo yake waliweza kushinda.
Hivyo basi ni wakati kwa wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia timu hiyo kwa hali na mali kuhakikisha inafanya vema katika michuano ya kombe la dunia na kuitoa kimasomaso Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Kwamba, jukumu la kuisaidia timu hiyo lisiachwe kwa viongozi tu wa chama husika bali liwe kwa kila mwenye nafasi ya kuchangia kufanya hivyo kwani hawa ni wawakilishi wa Tanzania na si chama binafsi.
Ifikie wahakati tuachane na kasumba ya kuthamini michezo kama soka au mpira wa kikapu tu kwa kuipa sapoti kubwa  pindi inaposhiriki mashindano mbalimbali huku michezo mingine ikidharaurika na wachezaji kuachwa kama watoto yatima.
Fikiria timu kama hiyo ya watu wenye ulemavu, kwa hali iliyokuwa nayo klakini imeweza kupambana kadiri ya uwezo wake na kuweza kushinda timu nyingine ambazo zilikuwa na sapoti kubwa toka kwa wananchi na viongozi wake.
Hiyo ni timu ya Watanzania wote na itakuwa fahari sana kama itaenda huko na kufanya vema na kuitangaza vema nchini.

Yaliyopita si ndwele tuanze sasa kwa timu hiyo na tusisubiri kuja kuipokea na kuandalia dhifa kubwa, kuialika bungeni  au Ikulu kama itatwaa ubingwa wa dunia wakati walihangaika peke yao katika maandalizi.