WASANII, WANAMICHEZO WATHAMINIWE


Na Dina Ismail
TANZANIA  ni moja ya  nchi zinazoaminika na kusifika  kuwa  na  watu wenye amani, upendo na ushirikiano.
Kweli!  tunasifika kwa hilo toka kwa watu wa nje, lakini kwa kiasi kikubwa hali hiyo haipo baina yetu katika baadhi ya makundi ya kijamii.
Tukiangalia  katika  sekta  ya sanaa na  michezo  suala la kutowathamini watu hao lipo na linaendelea kushika kasi kila kukicha.
Hapa kwetu,msanii au mchezaji anakuwa  anathaminiwa au kupendwa pindi  anapokuwa  mzima wa afya  na mwenye nguvu zake.
Tofauti na nchi za wenzetu ambazo hata kama zina machafuko lakini wasanii na wanamichezo wanathaminiwa katika hali zote mradi tu amepata kutoa mchango wa kisanaa na michezo katika nchi yake.
 Kwamba, kwa Tanzania thamani ya wasanii na wachezaji  inaonekana pindi wanakuwa katika uzima na afya njema lakini  wakipatwa na ugonjwa au umauti hakuna anayejali.
Tumeshuhudia mara kwa mara taarifa za wasanii na wanamichezo kuomba msaada wa matibabu wanapopata maradhi lakini mapokeo ya maombi yao huwa si ya kuridhisha.
Matokeo yake jukumu la kuuguza hubaki kwa wanafamilia na kwa bahati mbaya kuna wanaofikwa na umauti au kilema kutokana na maradhi yao na hakuna anayejali.
Kama hiyo haitoshi, kuna baadhi ya wachezaji wamejikuta wakikatiza ndoto zao baada ya kuumiwa wakizitumikia timu zao na bila huruma wanatelekezwa bila msaada wowote  kubaki wakijiuguza wenyewe.
Hili linasikitisha sana, kwani pamoja na mchezaji kuumia akiwa chini ya himaya yako bado unamuacha akahangaike kujitibia mwenyewe sasa hapo thamani yake iko wapi.
Kwamba, utaona ufahari kujitokeza katika msiba wake na kutangaza kuwasilisha kiasi kadhaa cha ubani,hilo hata mungu hapendi kwani kama mlikuwa mnamthamini mngemuhudumia kuanzia mwanzo mpaka pale ahadi yake itakapofika.
Hebu tuachane na roho za kikatili kwa watu wetu hawa kwani kwa namna moja ama nyingine wanasaidia kuitangaza nchi, wanasaidia kukupa wewe kula, wanasaidia kukupa  wewe heshima, wanatoa burudani, wanaelimisha na mengineyo mengi.
Pamoja na yote mazuri na michango yao katika jamii lakini hatuwathamini kama inavyostahili kulingana na waliyoyafanya wakati wa uzima au uhai wao.
Kama hiyo haitoshi, kuna wengine wanakumbwa na umauti na hata timu, taasisi au kundi alilokuwa akilifanyia kazi linashindwa hata kuhudhuria katika msiba wake.
Basi umeshindwa kuhudhuria msiba, mfano mchezaji huyo alipata kuwa tegemeo katika timu yako na kucheza kwa mafanikio leo anazikwa na timu yako inacheza lakini unashindwa hata kusimama kwa dakika moja tu kumuombea.
Watanzania tubadilike kwa kuthamini na kujali wenzetu!


Comments