BASATA INAWAJIBU WA KUREKEBISHA SHERIA NA KANUNI ZAKE ILI WASANII WASIKIUKE MAADILI YA NCHI


Na Dina Ismail
HIVI karibuni msanii wa muziki kipya nchini  Emmanuel Elibariki  maarufu kama ‘Na alitoa wimbo  uitwao ‘Wapo’ ambao  ulikuwa na mashairi makali kiasi cha kupelekea Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuufungia.
Awali msanii huyo alikamatwa na polisi kwa ajili ya mahojiano kutokana na mashairi yaliyopo katika wimbo huo ambayo yanadaiwa kuwasema viongozi wa Serikali, kabla ya Waziri wa Habari Utamaduni, sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kutaka achiwe huru.
Pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.John Magufuli naye akitoa zuio la wimbo huo huku akimshauri  auboreshe kwa kuongeza baadhi ya vipengele kadhaa ikiwemo  vinazozungumzia Wakwepa Kodi, Wauza Unga, Wabwia Unga, Wezi pamoja na watu wengine wasio na maadili mema katika jamii.
Nay msanii anayeimba muziki wake kwa mtindo wa Hip Hop amekuwa akikumbana na vifungo vya Basata mara kwa mara sambamba na kupewa onyo kutokana na nyimbo zake kukukiuka maadili ya Kitanzania.
Mara kwa mara Basata imekuwa ikiwakumbusha wasanii na wadau wa kazi kuzingatia maadili ya nchi sambamba na kufanya ubunifu wa hali ya juu kwa kutunga nyimbo zinazofikisha ujumbe kwa kufundisha , kuburudisha, kuelimisha na kuona.
Hiyo ni  kwa mujibu wa kifungu namba 4(L) cha sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, baraza limepewa jukumu la kusimamia kazi za sanaa na mamlaka kuhakikisha yote yanayofanyika katika sanaa hayaachi taifa na wasanii katika hali zisizo salama.
Hii ni mara ya tatu kwa Basata kuzifungia nyimbo za Nay kutokana na kukiuka maadili, ambapo kwa nyakati tofauti lilipata kuzifungia nyimbo zake zilizokwenda kwa jina ‘Shika Adabu Yako’ na ‘Pale Kati Patamu’.
Nay ni msanii mzuri sana, mwenye kujiamini  na mwenye kipaji cha hali ya juu, lakini kinachomuangusha ni matumizi ya lugha kali anazozitumia katika tungo zake ambazo mara nyingi zinaonekana kuwadhalilisha baadhi ya watu.
Hana woga, kwani kuna nyingine anafikia hatua hata ya kuwataja majina kabisa watu na hasa wasanii maarufu ambao wanafanya ndivyo sivyo katika jamii.Anafanya hivyo kwa lengo la kuwarekebisha.
Ni msanii muwazi kwani hata nyimbo alizoshiruikishwa nyingi amekuwa akitirika mashairi ya kupinga kitu flani ambayo ukiangalia kwa namna moja ama nyingine yanamaudhui mazuri tu.
Wengi hawamuelewi Nay na kumuona kama msanii mtukutu kitu ambacho sicho kwani Nay ni msanii anayependa mambo yaliyonyooka, yani hapendi ubabaishaji hivyo kuamua ‘kumwaga radhi’.
Pia nyota huyo, mara nyingi anapenda kutunga nyimbo kutokana na matukio ambayo yanakuwa yanatamba kwa kipindi hiko na hivyo akitoa wimbo mara nyingi unapokelewa kwa haraka sana na hivyo kuzidi kumuongezea umaarufu.
Ingawa  kwa upande mwingine Nay anatumia vibaya kipaji chake kwani kuna vitu vingine ni utashi wa mtu binafsi hivyo si vyema kumsema katika wimbo  kwa madai kuwa unamuweka sawa.
Ili kuepukana na utata kama wa Nay  na wasanii wengine wanaotoa kazi zisizo na maadili, ifikie wakati Basata ikarekebisha kanuni  na sheria zake katika kusimamia sheria na maadili ya nchini kwa kuweka muongozo mkali kwa wasanii wote iwe wa filamu au muziki.
Kwamba, ingeweka sheria kwa watayarishaji wote wa muziki na filamu kutokabidhi kazi za wasanii wanazozitayarisha mpaka zipitie Basata kwa ajili ya ukaguzi na ndipo wawakabidhi wasanii wenyewe na kuanza kuzitangaza katika vyombo vya habari.
Kama hiyo haitoshi, ingewetunga sheria kali ya kudhibiti hilo ili kulinda madili ya nchi  na kwa wale watakaokiuka sheria haina budi kuchukua mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine.
Nasema hivyo kwa sababu kuzuia wimbo ambao unakuwa umeshasambaa katika vyombo vya habari hakusaidii lolote, hivyo ni vyema udhibiti ungeanzia kwa watayarishaji  ili iwe rahisi kuwabana.

Pia Basata inawajibika kutoa semina za mara kwa mara kwa wasanii ili kuweza kuwakumbusha sheria, kanuni na maadili yanayopaswa kuzingatiwa wanapotayarisha kazi zao.