UKO WAPI MCHANGO WA WACHEZAJI WAKONGWE KATIKA SOKA HAPA NCHINI?Na Dina Ismail
MIAKA ya nyuma Tanzania ilipata kuwa na wachezaji wazuri sana ambao walidumu kwa muda mrefu katika mpira miguu na baada ya kustaafu  walijiendeleza na kuwa makocha.
Ubora na viwango walivyokuwa navyo ndio vinapelekea sasa hivi kujivunia  makocha kama  Charles Boniface Mkwasa, Fred Felix Minziro, Juma Mwambusi, Abdallah ‘King’ Kibaden, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ Salum Madadi, Sunday Kayuni  na wengineo.
Hawa kwa nyakati tofauti wamepata kuwa makocha wakuu wa timu kubwa kama vile Simba na Yanga, sambamba na kushika nyadhifa za juu za uongozi wa soka.
Kama hiyo haitoshi, wakongwe hao wamepata kuwa makocha wakuu ama wasaidizi katika timu za Taifa kwa nyakati tofauti katika miaka ya hivi karibuni.
Licha ya kuwepo kwa vipaji vingi hapa nchini lakini ukiangalia kwa haraka haraka kuna dalili ya kukosekana kwa makocha bora kama hawa katika miaka michache ijayo iwapo jambo hilo halitafanyiwa hamasa.
Kwamba, katika miaka ya hivi karibuni wachezaji wengi wazuri baada ya kustaafu waliamua kuachana na soka na kujikitika katika shughuli zao binafsi.Soka wanacheza tu kama ni sehemu ya mazoezi yao ya kawaida.
Wakali waliostaafu mwishioni mwa miaka ya 1990 mpaka 2010 ambao wamechukua kozi za ngazi mbalimbali za ukocha  kama Mohammed Mwameja, George Masatu, Ali Mayay, Mohammed  Hussein ‘Mmachinga’, Peter Manyika, Boniface Pawasa, Mussa mgosi, Nico Nyagawa na wengineo kama wangejikita katika ufundishaji naamini tungekuwa mbali.
Hawa walikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya timu zao hivyo naamini kama wangegeukia katika ukocha wangeweza kuzalisha na kuendeleza vipaji  vya vijana wanaoibuka kila kukicha.
Hongera kwa kina Suleiman Matola  na Mecky Mexime ambao  hawakutaka kuwa mchoyo wa kipaji vyao kwa kujiendeleza na taratibu walianza kuonesha mafanikio baada tu ya kustaafu kwa kuanza kufundisha timu zao.
Matola ambaye alipata kuichezea Simba na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa nyakati tofauti, baada ya kustaafu alianzia  kocha wa timu ya vijana ya Simba na kuiwezesha kutwaa ubingwa  wa kombe la Uhai, unaoshirikisha timu za vijana za Ligi Kuu Bara.
Matola pia ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa Ndanda Fc ya Mtwara, pia alipata kuwa kocha msaidizi wa  Simba, huku pia aliwahi kuifundisha  Geita Gold iliyokuwa  daraja la kwanza, hivyo akiendeleza juhudi zake atakuwa mmoja wa makocha bora zaidi katika miaka ya baadaye.
Kwa upande wa Mexime ambaye alipata kuichezea Mtibwa Sugar na Taifa Stars, baada ya kustaafu aligeukia ukocha ambako alianza kama kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar na baadaye kuwa kocha Mkuu.
Mexime kwa sasa ni kocha wa timu mwenza na Mtibwa, Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.
Tukirejea katika harakati za wachezaji wa zamani, bado ni kiza kinene kwani hata baadhi ya wanaojaribu kujiendeleza katika suala la ufundishaji bado hawajawa makini au kuamua kuwa makocha .
Kwamba, wengi wanasoma kwa ajili ya kupata vyeti  ili wapate kufundisha timu za mitaani na  zile za madaraja ya chini kitu ambacho hakiwezi kusaidia sana maendeleo ya soka.
Ingekuwa vema wakaiga mfano wa kina Mkwassa, Matola na Julio ili miaka ijayo tupate kuwa na watu wa kujivunia  na pia kusaidia kupunguza kasumba ya timu kuajiri makocha kutoka nje ya nchi.
Pia kwa hali iliyopo sasa hivi ambako wachezaji wengi vijana ambao hutamba sana na kutokana na umahiri wao lakini hupotea mapema katika medani hivyo kutishia kuwepo kwa hazina ya makocha kwa miaka ya baadaye.
Njia nyingine pia ya kuchangia maendelea ya soka ni kuanzisha vituo endelevu vya kuzalisha na kukuza soka la vijana  hapa nchini.
Na hiyo itawahusu hata wale wasiopenda  au kuwa na mwamko wa ukocha kuchangia kwa namna moja ama nyingine ukuzaji wa soka.Comments