YANGA KUENDELEZA UBABE KWA AZAM FC KESHO?

Young Africans kesho itashuka katika dimba la uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kupambana na wauza lamba lamba timu ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara 2013/2014.
Ikiwa imeshashuka dimbani mara nne na kuambulia pointi sita baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare michezo mitatu itashuka dimbani kuhakikisha inapata poniti 3 muhimu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa Ubingwa mara ya pili mfululizo.
Young Africans imerejea Dar es salaam siku ya alhamis ikitokea mkoani Mbeya ambako ilicheza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya timu za Mbeya Citiy na Prisons FC michezo iliyoishia kwa sare ya bao 1-1.
Katika kipindi cha mwaka mmoja Yanga imecheza michezo minne dhidi ya Azam FC na kushinda michezo yote ambapo mchezo wa kwanza ni fainali ya kombe la Kagame (2-0), Ligi Kuu mzunguko wa kwanza (2-0), mzunguko wa pili (1-0) na mechi ya ngao ya Hisani (1-0).
Takwimu zinaonyesha Young Africans wamekuwa wababe kwa timu ya wauza sembe kufuatia kuwa na mabao 6 ya kufunga katika michezo minne waliyokutana, huku ikizuia kabisa nyavu zake kutikiswa na Azam FC.
Hamis Kiiza anaongoza kwa kuifunga Azam FC mabao 3 katika michezo mitano aliyoichezea Yanga dhidi ya lamba lamba, huku washambuliaji Didier Kavumbagu na Said Bhanuzi wakifunga mara moja na viungo Haruna Niyonzima na Slaum Telela pia wakicheka na nyavu mara moja 
Kikosi chote kimeingia kambini katika hosteli zilizopo makao makuu ya klabu kujiandaa na mchezo huo wa jumamosi ambao ni muhimu kwa Young Africans katika kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
Kocha Mkuu Ernie Brandts amekuwa akiendelea kukinoa kikosi chake na kufanyia marekebisho mapungufu yaliyojitokeza katika michezo iliyopita kwa lengo la kuhakikisha hayatjitokezi tena katika michezo inayofuata.
"Tumetoka sare michezo mitatu, kikubwa nimekiandaa kikosi changu kuhakikisha kinaendeleza wimbi la ushindi dhidi ya Azam ukiwa ni mchezo wangu wa nne kama kocha kukutana na Azam huku nikiwa nimeshinda michezo mitatu yote iliyotangulia" alisema Brandts.
Tumetoka Mbeya salama nashukuru Mungu vijana wangu wote wapo fit na morali ni ya hali ya juu kuelekea mchezo huo na imani kwa mazoezi wanayondelea nayo kwa sasa kesho tutaibuka na ushindi katika mchezo huo "aliongeza Brandts" 
Aidha Brandts alisema anajua timu ya Azam FC ina kikosi kizuri ambacho kinatoa ushindani katika Ligi Kuu ya Vodacom lakini hiyo haitakua sababu ya kukizuia kikosi chake kuibuka na ushindi katika mchezo huo kwani Yanga ni timu bora na ina kikosi bora katika ukanda huu wa Afrika Maashariki. 
Wachezaji wote wameendelea na mazoezi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo huo: wachezaji waliopo kambini na wanaondelea kufanya mazoezi ni:
Walinda Mlango: Ally Mustapha 'Barthez', Deogratius Munishi 'Dida' na Yusuph Abdul
Walinzi wa Pembeni: Mbuyu Twite, Juma Abdul, David Luhende, Oscar Joshua na Issa Ngao
Walinzi wa Kati: Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani 'Cotton', Rajab Zahir na Ibrahim Job
Viungo Wakabaji: Athuman Idd 'Chuji', Frank Domayo na Bakari Masoud
Viungo Washambuliaji: Haruna Niyonzima, Hamis Thabit na Nizar Khalfani
Washambuliaji wa Pembeni: Saimon Msuva, Mrisho Ngassa na Abdallah Mguhi 'Messi'
Washambulijai: Hamis Kiiza, Jerson Tegete, Didier Kavumbagu, Hussein Javu, Said Bahanuzi na Shaban Kondo
Mchezaji pekee majeruhi ambaye ataukosa mchezo wa kesho ni kiungo  Salum Telela aliyeumia nyama za paja katika mchezo dhidi ya maafande wa jeshi la magereza Prisons jijini Mbeya kwa sasa anaendela na matibabu chini ya daktari wa timu Nassoro Matuzya.
CHANZO:www.youngafricans.co.tz

Comments