TEMEKE YAIZAMISHA RUKWA 5-1 COPA COCA-COLA

Temeke imejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza robo fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya leo (Septemba 10 mwaka huu) asubuhi kuizamisha Rukwa mabao 5-1. 
Hadi mapumziko katika mechi hiyo ya kundi B hatua ya Fainali za Taifa iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam, washindi walikuwa mbele kwa mabao 3-0. 
Mabao ya washindi yalitiwa wavuni na Constantine Katepa aliyefunga dakika ya 28, Patrick Ambrose dakika ya 36 huku Hamisi Kajole akipiga mawili dakika ya 43 na 71. Bao la nne lilifungwa dakika ya 46 na Ramadhan Juma.
 Rukwa ambayo kwa matokeo hayo imeshatolewa ilipata bao lake dakika ya 51 kupitia kwa Francisco Nkanga. Timu nyingine katika kundi hilo ni Geita na Ilala. 
Robo Fainali ya michuano hiyo itaanza keshokutwa (Septemba 12 mwaka huu). Kila kundi linatoa timu mbili kucheza hatua hiyo katika mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Coca-Cola.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)