TEMEKE, MJINI MAGHARIBI KUCHEZA NUSU FAINALI COPA

Temeke na Mjini Magharibi zinapambana kesho (Septemba 13 mwaka huu) katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 itakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam. 
Timu hizo zimetinga hatua hiyo baada ya kushinda mechi zao za robo fainali ya michuano hiyo zilizochezwa leo (Septemba 12 mwaka huu) asubuhi kwenye uwanja huo huo. 
Wakati Temeke imetinga hatua hiyo baada ya kuilaza bao 1-0 Iringa lililofungwa dakika ya 18 na Ramadhan Mohamed, Mjini Magharibi imeing’oa Mtwara kwa ushindi wa bao 1-0. 
Robo fainali nyingine zinachezwa leo (Septemba 12 mwaka huu) jioni kwa Kilimanjaro kuvaana na mabingwa watetezi Morogoro huku Arusha ikioneshana kazi na Ilala.