SIMBA KUKAMATA WANAOTUMIA NEMBO YAO, YAZINDUA MCHAKATO WA MAPENDEKEZO YA KATIBA

KLABU  ya Simba imewataka wafanyabiashara wanaotumia nembo ya klabu hiyo bila kuwa na kibali kujisalimisha kwa uongozi haraka iwezekanavyo, kinyume na hapo itawachukulia hatua kali za kisheria watakaokaidi agizo hilo.
"Kuanzia jumatatu kutakuwa na msako mkali ili kuwakamata wale wote wanaofganya biashara ya vitu vyenye nembo ya Simba bila ya kuwa na kibali,"amesema Ofisa habari wa Simba, ezekiel Kamwaga.
Kamwaga amesema leo kwamba tabia hiyo imekuwa ikiikosesha mapato klabu hiyo kutokana na ukweli kwamba, watu waliopewa mamlaka ya kuendesha biashara kwa kutumia nembo hizo wameshindwa kuziendesha baada ya watu wengine kuzalisha bidhaa zenye viwango vya chini na kuviuza kwa bei ya chini.
"Sisi tumetoa kibali kwa wafanyabiashara wawili tu ambao wao wanauza vitu orijino mfano jezi moja sh 25,000 lakini kuna watu wanatengeza jezi hafifu na kuuza kwa sh 7,000 ambapo watu wengi ndio wanazinunua hizo na kuikosesdha klabu mapato,"aliongeza kamwaga.
Katika hatua nyingine, klabu hiyo imezindua anuani maalum ya barua pepe kwa ajili ya wadau na wanachama kutoa mapendekezo yao ambayo wanahitaji yawemo kwenye katiba ya klabu hiyo.
Ameitaja anuani hiyo ni maoniyakatibaya Simba@gmail.com ambapo yatapokelewa hadi septemba 20 kabla ya kamati maalum kuyakusanya na kuyasambaza katika matawi na baadaye kurudi katika kamati hiyo ili yawekwe sawa kabla ya kuwasilishwa katika mkutano wa wanachama.