BAADA YA SARE TATU MFULULIZO YANGA WAJIPA MATUMAINI NA KUSEMA LIGI BADO MBICHI

MABINGWA watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara, Yanga Sc wamesema kutoka kwao sare katika mechi tatu mfululizo hakuwakatishi tamaa kwani ligi hiyo ndio kwanza ipo katika hatua za mwanzoni.
Kocha msaidizi wa Yanga Fred Felix Minziro amesema kwamba matokeo wanayoyapata ni sehemu ya mchezo hivyo yanawapa hamasa ya kuendelea kujifua zaidi sambamba na kurekebisha makosa ili wafanye vizuri katika michezo yao.
"Matokeo yanatokana na sababu mbalimbali, kama mechi zetu za Mbeya tatizo kubwa lililikuwa Uwanja hata ingekuwa timu gani isingeweza kuhimili hali ya uwanja ule,"alisema
Akienda mbali zaidi, Minziro alisema kwa ubovu wa viwanja vingi vya Tanzania kamwe ligi haitaendelea huku akiwasihi wadau kuhakikisha viwanja vinaboreshwa.
Aidha, minziro alisema timu nyingi ndogo zinazokutana na timu yake huwa zinaikamia sana kutokana na kuwa mabingwa watetezi, hivyo amewataka wadau na mashabiki wa Yanga kutulia kwa sasa na kuendelea kuisapoti timu yao kwa namna moja amba nyingine.
Mabingwa hao watetezi juzi walilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji Tanzania Prisons,huku awali walitoka sare kama hiyo na Mbeya City na Coastal Union ya Tanga.