UDE UDE:MWENYE KIPAJI CHA UTUNZI WA NYIMBO AMBAZO ZIMEWAPA TUZO NYOTA KAMA LADY JD,QUEEN DARLIN

LICHA ya nyimbo alizowatungia baadhi ya wasanii nyota wa muziki wa bongo fleva kutwaa tuzo, lakini kazi anazozitoa mwenyewe hazijaweza kumpa umaarufu mkubwa kama kipaji alicho nacho.
Huyo si mwingine, bali ni msanii wa muziki wa bongo fleva, Hamidu Hafidh Mshinda maarufu kama Ude Ude.
Nyimbo kama ‘Wangu’ ya Lady Jaydee, ‘Maneno Maneno’ ya Queen Darleen, ‘Bwashee’ ya Baby J, ‘Oyoyo’ Bob Junior na nyinginezo ni baadhi tu ya nyimbo ambazo zimetungwa na Ude Ude na kutwaa tuzo mbalimbali.
Baada ya kuwawezesha wasanii wenzake kwa tungo nzuri, kwa sasa Ude Ude ameamua kuweka kando suala la kuwatungia nyimbo wasanii wengine na sasa kujikita mwenyewe katika uimbaji.
Katika mkakati huo, mwanzoni mwa wiki hii ameachia ‘singo’ yake mpya inayokwenda kwa jina la ‘Ngoma Inogile’, iliyotengenezwa katika studio za Fire Music chini ya mtayarishaji More Fire.
Kama hiyo haitoshi, Ude Ude anatarajia kuizindua rasmi video ya wimbo huo, Iddi Mosi ndani ya ukumbi wa kimataifa wa Club Bilicanas uliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii, Ude Ude anaeleza kwamba, kwa sasa amejipanga vema kuhakikisha anafika kileleni katika medani ya muziki wa bongo flava.
“Nimedhamiria vilivyo kuliteka soko la muziki kwa sasa, tofauti na zamani ambapo nilikuwa natoa nyimbo tu kama kujifurahisha, nimejipanga vema, hivyo naomba mashabiki mnipokee,” anasema.
Ikumbukwe kuwa kabla ya singo yake hii mpya, Ude Ude alipata kutoka na nyingine kadhaa, zikiwemo ‘Kujinafasi’ alioutoa mwaka 2009 na ‘Nipe Kidogo’ mwanzoni mwa mwaka huu.
Akifafanua zaidi, Ude Ude anasema tayari ana nyimbo zaidi ya 60 ambazo amezitayarisha katika studio tofauti, huku akiwashirikisha wasanii mbalimbali ili kuleta ladha na vionjo tofauti, ambapo hivi sasa yuko chini ya usimamizi wa Kampuni ya Babuu Kisauji Entertainment.
Akizungumzia safari  yake kimuziki, Ude Ude anasema ilianzia mwaka 2002 akiwa na ndugu yake aitwaye Ramadhan Yusuf, ambaye alikuwa akimfundisha jinsi ya kuandika huku jioni wakifanya mazoezi ya kuimba katika saluni moja karibu na nyumbani kwao.
Anasema mwaka 2004 alishiriki mashindano ya muziki yaliyoandaliwa na msanii wa filamu, Dk. Cheni katika ukumbi wa Da West Park Tabata, akiwa na kundi la Kyudas lililoundwa na wasanii Big Black na Kg Son na kujikuta wakishinda na kuzawadiwa sh 100,000.
“Baada ya mashindano hayo, nilitulia kabla ya mwaka 2009 kutoka na singo yangu ya kwanza niliyoipa jina la ‘Kujinafasi’ ambayo iliweza kunitambulisha katika medani ya muziki, ingawa kwa kiasi kidogo sana,” anasema.
Anasema aliendelea kujikita katika kuwatungia wasanii wenzake nyimbo kabla ya kukutana na meneja wake wa sasa, Babuu Kisauji, ambaye alianza kumpa ushauri na ndipo mapema mwaka huu, akaachia singo nyingine iitwayo, ‘Nipe Kidogo’.
Ude Ude anasema kutokana na kuwa chini ya usimamizi maalumu, sambamba na kujipanga katika kufanya vema kwenye medani ya bongo fleva, ameweka pembeni suala la kutungia wasanii wenzake, badala yake atafanya hivyo kwa mkataba maalumu.
Akiwa na matarajio ya kufika mbali zaidi na kuwasaidia wasanii wengine, Ude Ude amewataka kupendana na kushirikiana, huku akiwasisitiza waliopiga hatua kupambana kimataifa badala ya kukaa wakiwadhibiti chipukizi.
“Waliopiga hatua waangalie mbele kwa kutafuta soko nje ya mipaka si kukabana na chipukizi, pia tuwe wabunifu, kwani itatusaidia kusonga mbele na wadau wa muziki watoe sapoti kwa wasanii wote, si kuangalia huyu anafanya kazi  na nani,” anaongeza.
Ude Ude ambaye anavutiwa na msanii Suma Lee, alizaliwa Machi 3, 1988 jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi Shule ya Ilala.
Hata hivyo hakuendelea na masomo kutokana na matatizo ya kifamilia, hasa kukosa mtu wa kumlipia ada kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu.


Comments