UCHAGUZI MKUU TFF KIZA KINENE

Na Dina Ismail 
UWEZEKANO wa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufanyika ndani ya kipindi kilichotakiwa na Shirikisho la soka Tanzania (Fifa), ni mdogo, Tanzania Daima imebaini.
Wakati Fifa wakiagiza uchaguzi huo uwe umefanyika ifikapo Oktoba 30, lakini marekebisho ya katiba yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa Dharura Julai 13, yamekwama katika
Ofisi ya Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo.
Japo TFF imepanga uchaguzi huo ufanyika Septemba 29, lakini suala la Katiba hiyo kukwama kwa Msajili, kunatia shaka kama uchaguzi huo utafanyika kwa ulitakiwa na Fifa
Wakati kukiwa na ukimya huo, habari zilizoifikia Tanzania Daima, zinasema kukwama kwa Katiba hiyo katika ofisi ya Msajili, ni kutokana na dosari mbili kubwa zilizofanywa.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa, dosari ya kwanza ambayo imeifanya ofisi ya Msajili kusita kupitisha marekebisho hayo, ni staili iliyotumiwa na Mkutano Mkuu kuipitisha Katiba hiyo.
Kwamba, wakati Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Shirikisho hilo ikitaka marekebisho yapigiwe kura, kuna habari kuwa jambo hilo halikufanywa na wajumbe wa mkutano Mkuu.
Kwa mujibu wa kipengere hicho, ili marekebisho yawe halali, yapaswa kupata baraka ya zaidi ya asilimia 50 ya idadi ya Wajumbe katika mkutano huo.
“Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya TFF inatamka wazi ili marekebisho yaweze kuwa halali, yanapaswa kupata baraka ya asilimia 50 + 1 ya wajumbe walipo ukumbini. Katika uchaguzi ule wa Julai 13, hili halikufanyika, ilipitishwa kijumla tu,” kilidokeza chanzo chetu. 
Habari zinasema, kwa vile jambo hilo halikufanyika katika upitishaji wa marekebisho hayo, Ofisi ya Msajili imejikuta kwenye wakati mgumu kuipitisha hadi kufikia jana, akihoji ilipitishwa kwa staili ipi kwani utaratibu ni wajumbe kupiga kura.
“Ili marekebisho yaweze kuwa halali, yanapaswa kuuungwa mkono na asilimia 50+ 1 ya idadi ya wajumbe waliohudhuria mkutano husika,” kinasomeka kifungu hicho cha tatu cha Ibara ya 30 ya Katiba ya shirikishi hilo.
Habari zinasema, japo Ofisi ya Msajili ingependa kuona mchakato wa uchaguzi huo unafanyika ndani ya kipindi kinachotakiwa na Fifa, lakini dosari hiyo imeifanya isite kuipitisha katiba hiyo haraka kama ilivyokuwa imetarajiwa.
Kinachotishia zaidi uchaguzi huo kufanyika kwa wakati, ni mchakato mzima kuhitaji muda wa siku zisizopungua 60 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, hivyo kama si rasimu hiyo kukwama kwa Msajili, mchakato huo ungepaswa uwe umeanza walau kuanzia leo.
Aidha, kitendo cha Kamati ya Utendaji kufanya uteuzi wa Kamati mbalimbali kwa mujibu wa marekebisho yaliyomo kwenye rasimu inayosubiri baraka za Msajili, ni dosari nyingine ambayo
pia imehojiwa na Ofisi ya Msajili.
“Ofisi ya Msajili imehoji pia uundwaji wa Kamati za Maadili umefanywa kwa katiba ipi? Inajiuliza hivi kwa sababu marekebisho yaliyofanywa bado hayajapata baraka kisheria,” kilisema chanzo hicho.  
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Msajili, Mercy Rwezaura kupata kauli yake
juu ya madai hayo, alisema hawezi kusema lolote kwa vile ofisi yake bado inaendelea kuipitia.
“Kwa sasa siwezi kusema lolote kwa vile bado tunaendelea kuipitia,” alisema Msajili huyo.
Alipoulizwa juu ya madai kwamba dosari ndizo zimeifanya ofisi yake ishindwe kupitisha rasimu hiyo kwa wakati, alisema hana taarifa yoyote na kusisitiza  wanaendelea kuipitia rasimu ya katiba hiyo.
Tanzania Daima lilimtafuta Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kujua mustakabali mzima wa katiba na mchakato wa uchaguzi huo kwa ujumla, alisema bado wanasubiri majibu kutoka kwa msajili kabla ya mengine kuendelea.
Kuhusu madai ya dosari ya akidi, Osiah alisema wakati wa kukabibidhi marekebisho hayo kwa Msajili, waliambatanisha na muhtasari wa mkutano huo ambao unaonesha kila kitu kilichofanywa na wajumbe wa Mkutano Mkuu.
“Katika katiba tuliyoipeleka kwa Msajili, tuliambatanisha muhtasari ya wajumbe walioshiriki, sasa sijui idadi ipi inayohojiwa,” alisema
Kuhusu uteuzi wa Kamati mbili mpya za Maadili, Osiah alisema kwa mujibu wa katiba hiyo hiyo ya TFF, mabadiliko yaliyopitishwa huanza kutumika mara moja hata kabla ya kupitishwa na Msajili.
Awali, uchaguzi wa Shirikisho hilo ulipangwa kufanyika Februari 24, mwaka huu, lakini ukaota mbawa baada ya Shirikisho la Soka kutaka iwe hivyo kutokana na
baadhi ya wagombea kulalamika kuchujwa isivyo halali.
Baada ya Fifa kumtuma mjumbe wake, Primo Carvaro kuja nchini na kupeleka ripoti, ndipo Shirikisho hilo lilipoagiza uundwaji wa Kamati mbili za Maadili na kutaka uchaguzi uwe umefanyika hadi ifikapo Oktoba 30.
Hata hivyo, habari zinasema pamoja na dosari hizo, Ofisi ya Msajili yaweza
kuipitisha katiba hiyo kwa sharti la dosari hiyo kifanyiwe kazi katika Mkutano
Mkuu wa Uchaguzi kama ilivyokuwa uchaguzi wa Desemba 27, 2004.

Comments