SIMBA YAWATOSA YANGA SAKATA LA AZAM TV


UONGOZI wa klabu ya Simba, umesema haki ya kurusha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kumilikiwa na Azam TV ni ukombozi wa kiuchumi kwa klabu shiriki na maendeleo ya soka hapa nchini.
Tamko la Simba, moja ya klabu kongwe nchini, limekuja siku chache tangu watani wao Yanga, wakatae udhamini huo kwa hoja mbalimbali, ikiwemo mchakato wa jambo hilo kutowekwa wazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema wanaridhia hilo kwa sababu hata kanuni za vyombo vya juu vya mchezo huo, kama Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Afrika (CAF), na Tanzania (TFF), ndivyo vyenye haki ya kufanya majadiliano juu ya matangazo ya kwenye televisheni.
Alisema kwa muda mrefu klabu zimekuwa zikilalamika kutokuwepo wadhamini, sasa litakuwa jambo la ajabu timu ipinge udhamini huo kwa sababu ambazo hazina mashiko.
Kamwaga alikwenda mbali na kuhoji, hao wanaopinga udhamini wa Azam Tv, walikuwa wapi kufanya hivyo wakati SuperSport ya Afrika Kusini ikionyesha baadhi ya mechi za ligi hiyo bure?
“Tulikuwa na SuperSport kwa miaka kadhaa wakionesha michezo yote, tena buree…leo hii Azam Tv wanakuja na sh milioni 100, tunaanza kuleta mizengwe, tunadhani si jambo zuri,” alisema Kamwaga.
Kamwaga alisema kutokana na umuhimu wa udhamini huo, klabu zinapaswa kuikumbatia Azam Tv, kwani utasaidia kuvuta kampuni nyingine kuwekeza kwenye ligi hiyo.
Alisema kama kuna tatizo la kuzungumza kuhusiana na udhamini huo, wasizungumzie pembeni, hasa ikizingatiwa kuwa mchakato mzima ulihusisha pia Bodi ya Ligi chini ya Mwenyekiti wake, Wallace Karia.
Katika hatua nyingine, Simba inatarajiwa kushuka Uwanja wa Taifa kesho kukwaana na kombaini ya polisi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 24.
Mechi hiyo itakayoanza saa 10 jioni, viingilio ni sh 20,000 kwa VIP A, 15,000 VIP B, 10,000 VIP C na 5,000 kwa viti vya kijani, chungwa na bluu.