HALI SI SHWARI NDANI YA KLABU YA SIMBA, MGOMO WA CHINI CHINI WAFUKUTAHAMKANI hali si shwari ndani ya klabu ya Simba ambapo kama uongozi usipochukua hatua za haraka basi itakuwa ni ndoto kwa timu kufanya vema kwenye ligi kuu soka Tanzania Bara iliyoanza kutimua vumbi jumomosi iliyopita.

Hiyo inatokana na kuwepo kwa mgomo baridi unaoendelea ndani ya kikosi cha Simba ambao unatokana na tabaka lililowekwa baina ya wachezaji ambapo kuna makundi mawili, lile la wanaopangwa na wasiopangwa kwenye mechi.
Habari za uhakika toka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kwamba hali hiyo imekuwa ikiota mizizi kadiri siku zinavyosonga kiasi hata walipokwenda Tabora kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza dhidi ya Rhino ya huko, makundi hayo yaliwewkwa katika hoteli tofauti.
Imeelezwa kuwa, hali hiyo imekuwa ikivunja ushirikiano kama timu baina ya wachezaji pindi wawapo uwanjani hali ambayo inachangia kuwa na matokeo ya kutoridhisha katika michezo yake.
“Hili halijaanza jana wala juzi ni muendelezo tu, hata katika mchezo wa Rhino sare ile ni matokeo ya mgawanyiko huo ambao umesababisha kuondoa morali ya wachezaji uwanjani na matokeo yake timu inacheza tu kutimiza wajibu,”kilieleza chanzo cha habari hiyo
Aidha, mtoa habari huyo alisema kama uongozi hautakuwa makini kutatua suala hilo itakuwa vigumu kwa timu kufanya vema katika michezo yake inayofuata katika ligi hiyo na mingineyo.

Simba ambayo kwa sasa ipo jijini Arusha tayari kwa mchezo wake dhidi ya JKT Oljoro ya huko utakaopigwa kesho kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid mjini humo, iliianza ligi hiyo Agosti 24 kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino ya Tabora mchezo uliopigwa dimba la Ali Hassan Mwinyi.