KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari,
imejitosa kudhamini Chama cha Darts Tanzania (Tada) katika mashindano ya mchezo
huo kwa timu za Jeshi la Wananchi(JWTZ), Polisi na Magereza ‘Majeshi Challenge Cup’ ambapo pia imedhamini
mashindano ya Jeshi la Wananchi pekee yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai
5 hadi 7 mwaka huu katika ukumbi wa Jeshi la Wananchi, Msasani jijini Dar es
Salaam.
Meneja wa Bia ya Safari, Oscar Shelukindo alisema mashindano
hayo yatakuwa ya kila mwaka kwakuwa wameamua kudhamini mashindano hayo ili
kuinua mchezo wa Darts, kuhamasisha na kuburudisha majeshi nchini.
Alisema thamani ya udhamini wa mashindano hayo likiwemo la
Jeshi la Wananchi pekee litakalo julikana kama
Ngome Darts Challenge ni sh. Milioni 16 na laki mbili ambapo fedha hizo ni
kwamichuano yote miwili ikijumuisha zawadi, maandalizi na gharama za kuendesha
mashindano.
“TBL kupitia bia ya Safari tumeamua kudhamini mashindano
haya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mipango yetu kuendeleza michezo na
kushiriki katika shughuli za kijamii hapa nchini ambapo huu ni mwaka wa tatu
mfululizo kwa kampuni yetu kupitia bia ya Safari kudhamini mashindano mbali
mbali ya Darts nchini na hata katika ukanda wa Afrika Mashariki” alisema
Shelukindo.
Katika Mashindano ya Darts kombe la Majeshi yaliyoanza
kutimua vumbi Juni 28 na kuhitimishwa juzi, timu ya Lugalo ilijinyakulia kitita
cha sh. 500,000 baada ya kuibuka bingwa wa mashindano hayo huku Polisi Barack
wakijinyakulia sh. 300,000 baada ya kukamata nafasi ya pili ambapo washindi wa
tatu na nne Polisi Barack A na Ngome Dar es Salaam wakijinyakulia kitita cha
sh. 150,000 ambapo washiriki wengine kutoka Polisi Mbeya, na Mzinga wakiondoka
na kifuta jasho cha sh. 100,000 pamoja na zawadi za vikombe, fulana, na ndara
kwa washiriki wote.
Naye Katibu wa Tada, Kale Mgonja aliwashukuru TBL kupitia
bia ya Safari kwa kuweza kufanikisha mashindano hayo ambapo wanaamini
mashindano yajayo yatakuwa na ubora zaidi katika kuuendeleza mchezo huo kote
nchini.
Comments
Post a Comment