MABINGWA wa soka Tanzania
Bara na Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC leo wameanza rasmi mazoezi bila ya
kocha wake mkuu, Ernie Brandts ambayo ameshindwa kurejea nchini juzi kama
ilivyopangwa.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga
walifanya mazoezi hayo katika Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo,
Dar es Salaam chini ya kocha msaidizi Freddy Felix Minziro.
Ofisa habari wa Yanga Baraka Kizuguto amesema kwamba karibu
wachezaji wote waliopo nchini walihudhuria mazoezi hayo.
Alisema kocha Brandts ambaye
alikuwa kwao kwa ajili ya mapumziko alishindwa kuwasaili nchini juzi
anatarajiwa kuwasili wakati wowote na kuendelea na majukumu yake ya kukinoa
kikosi hicho.
Aliongeza kuwa kwa sasa
wachezaji hao watakuwa wakifanya mazoezi ya kawaida huku wakiwasubiri wachezaji
wengine waliomo katika timu za Taifa ambazo zinajiandaa na mechi za kufuzu
fainali za kombe la Dunia zitakazopigwa mwishoni mwa wiki hii.
Wachezaji wa Yanga waliopo
kwenye timu za Taifa ni pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mrisho Ngassa, Ali
Mustafa ‘Barthez’ Frank Domayo, Simon Msuva na Athuman Iddi ‘Chuji’ ambao wapo
katika kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa kwa ajili ya mchezo wake na
Morocco.
Wengine ni wachezaji wa
kimataifa Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite waliopo timu ya Taifa ya Rwanda
‘Amavubi’ na Hamis Kiiza aliyepo kikosi cha Uganda ‘The Cranes’.
Yanga, Simba na Super Falcon
ya Zanzibar zitashiriki michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi
kuanzia Juni 18 hadi Julai 2 huko Sudan Kusini.
Mabingwa hao watetezi
wamepangwa kundi C pamoja na Vital’O ya Burundi, Express ya Uganda na Ports ya Burundi ambapo wataanza kutetea
taji lao juni 20 kwa kucheza na Express.
Comments
Post a Comment