WAALGERIA KUCHEZESHA TAIFA STARS, IVORY COAST

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua waamuzi kutoka Algeria kuchezesha mechi kati ya Taifa Stars na Ivory Coast itakayofanyika Jumapili saa 9 alasiri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Waamuzi hao watakaochezesha mechi hiyo ya kundi C kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil wataongozwa na Charef Mehdi Abid atakayepuliza filimbi. Atasaidiwa na Hamza Hammou na Bouabdallah Omari wakati mezani atakuwa Sofiane Bousseter. 
Abdi na wezake wanatarajiwa kutua nchini Ijumaa (Juni 14 mwaka huu) saa 12 asubuhi kwa ndege ya EgyptAir. Mtathmini wa waamuzi ni Athanase Nkubito kutoka Rwanda ambaye atatua nchini Ijumaa (Juni 14 mwaka huu) saa 12 jioni kwa ndege ya RwandAir. 
Kamishna wa mechi hiyo ni Bernard Mfubusa kutoka nchini Burundi ambapo atawasili nchini Ijumaa (Juni 14 mwaka huu) saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways. Maofisa wote hao wa mechi hiyo watarejea makwao Jumatatu (Juni 17 mwaka huu).

HATUA YA TATU RCL KUCHEZWA JUMAMOSI
Mechi za kwanza za hatua ya tatu ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao zitachezwa Jumamosi (Juni 15 mwaka huu) wakati za marudiano zitachezwa Jumatano ya Juni 19 mwaka huu.

Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana leo (Juni 11 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za michezo iliyopita na kufanya uamuzi mbalimbali ikiwemo mechi ya marudiano kati ya Mpwapwa Stars na Machava FC ambayo haikuchezwa. 
Machava FC ambayo ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Moshi kwa mabao 2-0 inaendelea katika hatua ya tatu kwa vile haikuhusika katika kukwamisha mchezo wa marudiano uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. 
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kiliuhamishia mchezo huo kwenye Uwanja wa Mgambo mjini Mpwapwa kinyume na maelekezo ya Kamati ya Mashindano ya TFF. Kamati katika kikao chake cha awali iliekeleza kuwa mechi zote za RCL zitachezwa makao makuu ya mikoa isipokuwa kwa Morogoro ambapo timu ya Techfort FC iliruhusiwa kutumia Uwanja wa CCM Mkamba mjini Ifakara. 
Hivyo timu nane zilizofuzu kucheza raundi hiyo ni Friends Rangers ya Dar es Salaam, Kariakoo ya Lindi, Katavi Warriors ya Katavi, Kimondo SC ya Mbeya, Machava ya Kilimanjaro, Njombe Mji ya Njombe, Polisi Jamii ya Mara na Stand United FC ya Shinyanga. 
Wakati timu nyingine zimefuzu kwa kushinda mechi zao za raundi ya mbili, Njombe Mji imeingia hatua hiyo kwa kuwa timu yenye uwiano mdogo wa kufungwa (best looser) katika hatua ya pili. 
Katika hatua hiyo mechi ni ifuatavyo; Kariakoo vs Friends Rangers, Machava FC vs Stand United FC, Polisi Jamii vs Katavi Warriors, na Kimondo SC vs Njombe Mji. Timu zilizoanza kutajwa ndizo zinazoanzia nyumbani. 
Vilevile Kamati ya Mashindano imeagiza Kamishna wa mechi ya marudiano kati ya Mpwapwa Stars vs Machava FC, Mwijage Rugakingira wa Tanga ambaye alikwenda Uwanja wa Mgambo badala ya Uwanja wa Jamhuri kinyume na maelekezo ya TFF aondolewe kwenye orodha ya makamishna.

Pia waamuzi wa mechi hiyo ambao nao walikwenda Mpwapwa badala ya Dodoma Mjini wamepelekwa Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kutokana na tukio hilo.

Kamati ya Mashindano imekumbusha kuwa RCL ni mashindano yanayosimamiwa na TFF, hivyo maelekezo yoyote kuhusiana na mashindano hayo pia yatatoka TFF na si mahali pengine popote. Hivyo, msimamizi wa kituoa hana mamlaka ya kubadili uwanja.

Hatua ya nne ya RCL itachezwa kati ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 29 na 30 mwaka huu.

Comments