SIMBA, YANGA ZIKO NJIA PANDA KOMBE LA KAGAME

WAKATI baadhi ya timu zikitangaza kujitoa katika michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kagame’, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano hiyo timu za Simba na Yanga zimesema zinasubiri tamko toka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). 
Hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa machafuko katika jimbo la Darfur nchini Sudan ambapo michuano hiyo imepangwa kufanyika kuanzia Juni 18 hadi Julai 2 huko Sudan Kusini. 
Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana, viongozi wa juu wa vilabu hivyo, walisema kwamba hali inayoendelea Sudan inawatia hofu lakini suala la kushiriki ama kutoshiriki lipo mikononi mwa Tff. 
Katibu Mkuu wa Yanga Lawrance Mwalusako alisema jana kwamba wao Tff kama wasimamizi wa soka hapa nchini hawana budi kufuatailia hali hiyo na kutoa tamko rasmi. 
Alisema kama wanachama hawawezi kuamua kujitoa kwenye michuano hiyo kwani kuna mamlaka husika (Tff) inayowajibika kufuatilia mwenendo mzima ikiwemo hali ya usalama. 
“Tupo chini ya Tff  hivyo hatuwezi kuamua kujitoa bila ya kupata baraka kutoka kwao, ni wajibu wao kufuatilia hali halisi kwanza na kutoa tamko juu ya ushiriki wetu,”alisema Mwalusako 
Naye Makamu Mwenyekiti wa Simba  Joseph Itang’are ‘Kinesi’ alisema pamoja kuwepo na hali tete nchini Sudan bado wanasikilizia maamuzi ya mamlaka za juu (Tff) juu ya hatma ya ushiriki wao. 
Alisema kama washiriki wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo mpaka pale itakapojulikana mustakabali mzima wa mashindano hayo na hali halisi ya nchini Sudan. 
“Tunaiomba TFF kulitilia maanani suala hili na kutoa tamko hili, sisi hatuwezi kujiamualia tu wakati kuna chombo husika kinachotuongoza,”alisema 
Katika hatua nyingine, kocha mkuu wa Yanga Ernie Brandts ametua nchini juzi na leo anatarajiwa kuanza kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na michuano ya Kagame. 
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, walianza mazozi mapema wiki hii kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola chini ya kocha msaidizi Fred Felix Minziro.

Comments