MKUTANO MKUU MAALUM WA MAREKEBISHO YA KATIBA YA TFF KUFANYIKA JULAI 13

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa notisi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho utakaofanyika Julai 13 mwaka huu kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam ukiwa na ajenda moja ya marekebisho ya Katiba. 
Notisi hiyo imetolewa juzi (Juni 12 mwaka huu). Rais ameitisha Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(1) ya Katiba ya TFF baada ya kupata maagizo kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa barua yake ya Aprili 29 mwaka huu. 
Ajenda rasmi na taarifa nyingine zitatumwa kwa wajumbe siku 15 kabla ya Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(4) ya Katiba ya TFF. Wanachama wa TFF ambao ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu wanatakiwa kutuma majina ya wajumbe halali. 
TFF inapenda kuwakumbusha wanachama wake kutuma majina ya wajumbe halali ili kufanikisha maandalizi ya Mkutano huo. Ni vizuri kuhakikisha kuwa jina linalotumwa ni la mjumbe halali wa Mkutano Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya TFF.

RCL YAINGIA HATUA YA TATU WIKIENDI HII
Mechi za kwanza za hatua ya tatu ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao zinachezwa wikiendi hii kwenye viwanja vinne tofauti. 
Mechi za kesho (Jumamosi) ni kati ya Kariakoo ya Lindi na Friends Rangers ya Dar es Salaam utakaochezwa katika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi wakati Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya wenyeji Kimondo SC na Njombe Mji. 
Timu za Machava FC ya Kilimanjaro na Stand United FC ya Shinyanga, Polisi Jamii ya Mara na Katavi Warriors ya Katavi zilizokuwa zipambane kesho mechi zao zimesogezwa mbele hadi keshokutwa (Jumapili). Mechi hizo zimesogezwa kutokana na viwanja vya Ushirika mjini Moshi na Karume mjini Musoma kuwa na shughuli nyingine za kijamii. 
Hata hivyo, TFF imesisitiza kuwa ikibainika kuwa viwanja hivyo havikutumika kwa shughuli za kijamii siku hiyo ya Jumamosi, hatua kali zitachukuliwa kwa wanachama wake (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa husika). 
Mechi za marudiano za hatua hiyo ya tatu zitachezwa Juni 19 mwaka huu. Hatua ya nne ya RCL itachezwa kati ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 29 na 30 mwaka huu.

Comments