JK AWAPA MOYO STARS,NGASA KUIKOSA IVORY COAST J'2

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inayodhamini Timu ya Taifa (Taifa Stars) akisalimiana na Nahodha wa Taifa Stars Juma Kaseja wakati wa hafla fupi ya kuzungumza na wachezaji jana kabla ya mechi dhidi ya Ivory Coast. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete amewataka wachezaji wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kucheza kwa nguvu zote kesho dhidi ya Ivory Coast na hatimaye kuibuka na ushindi. 
Stars na Ivory Coast zitakwaana keshokutwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la Dunia zitakazopigwa mwakani nchini Brazil. 
Akizungumza kwa niaba ya Rais, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mecky Sadick alisema kwamba, Kikwete aliridhishwa na mchezo waliounyesha walipokwaana na Morocco wiki iliyopita licha ya kufungwa mabao 2-1. 
Alisema anaamini kikosi cha Stars kipo tayari kwa mchezo huo baada ya kufanya maandalizi mazuri hivyo kazi iliyobaki ni kutumia vema uwanja wa nyumbani hiyo kesho na kushinda. 
“Rais amenituma kwenu nije kuwaambia kwamba alifurahishwa na jinsi mlivyocheza dhidi ya Morocco wiki iliyopita, pamoja na kufungwa kwenu amekisifu kikosi hiki hivyo amewataka kutokata tamaa katika mchezo wenu wa Jumapili,”alisema Sadick 
Awali, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah amesema kwamba kikosi cha Stars kilichopiga kambi kwenye Hoteli ya Tansoma kipo tayari kwa mchezo huo, huku akiwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia.  

Aidha, kiungo wa Stars Mrisho Ngasa naye kesho ataukosa mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi mbili za njano.