AMRI KIEMBA NDIYE MWANASOKA BORA TANZANIA

Na Hosea Joseph
 KIUNGO mahiri wa Simba na timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Amri Kiemba, juzi alitwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka katika hafla iliyofanyika chini ya uratibu wa Umoja wa Wanasoka Tanzania (Sputanza), kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Mbali ya Kiemba, mchezaji Salum Abubakar ‘Sure boy’ wa Azam FC alitwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa mwaka, huku Kocha wa Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro, Mecky Maxime akibeba tuzo ya Kocha Bora huku kipa bora akiwa ni Hussein Sharif, pia wa Mtibwa.
Tuzo hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza kwa lengo la kuongeza ushindani kwa wachezaji kwenye klabu zao na timu za taifa, imefanyika chini ya udhamini wa Kampuni ya Kishen Enterprises Ltd katika vigezo vya nyota bora wa mwaka, chipukizi bora na kocha bora na kipa bora.
Kiemba aliibuka mshindi wa tuzo hiyo akiwabwaga Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu wote wa Yanga, Kipre Tchetche (Azam FC) na mshambuliaji Paul Nonga wa JKT Oljoro.
Kwa upande wa Sure boy, alitwaa tuzo yake akiwabwaga Hassan Dilunga wa Ruvu Shooting, Idrisa Rashid wa Yanga, Frank Sekula na  Shomari Kapombe wa Simba.
Mexime alijitwisha tuzo akiwashinda Charles  Boniface Mkwasa wa Ruvu Shooting, Abdallah Kibadeni wa Kagera Sugar na Jumanne Chale wa Tanzania Prisons. Sharif aliwashinda kipa namba moja wa Simba na Stars, Juma Kaseja na Mwadin Ally wa Azam FC.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Sputanza, Musa Kisoki alisema washindi wa tuzo hizo wamepatikana baada ya uteuzi na upigwaji kura uliofanywa na makocha na manahodha wa timu mbalimbali nchini.
Alisema vigezo vilivyotumiwa ni sifa ya mchezaji, nidhamu ya ndani na nje ya uwanja, mafanikio yake kwenye klabu yake, uwezo wake binafsi na mambo mengine yanayofanana na hayo na akawashukuru wote walioshiriki kwa namna mbalimbali kufanikisha tuzo hiyo.
“Nawashukuru waliofanikisha tuzo hizi na wote mliofika kwani huu ni mwazo, lakini naamini tutafikia mafanikio makubwa katika maandalizi mengine badae yanayokuja kwa kuwa kila jambo huwa gumu mwanzoni,” alisema Kisoki.
Alisema tuzo hizo zitakuwa zikitolewa kila mwaka chini ya udhamini wa Toyo ili kuwaongezea wachezaji na makocha ari uwanjani wakati wa mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa viongozi walioshudhuria hafla hiyo ni Mama Salma Kikwete aliyekabidhi zawadi za pikipiki na vyeti vya kuwakumbuka na kuwapongeza wachezaji wakongwe wa zamani waliochezea timu ya taifa miaka ya nyuma.
Naye mgeni rasmi katika tuzo hizo, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani aliwasihi Sputanza kuwasaidia wachezaji katika vita ya dawa za kulevya na vitendo vya rushwa kwa ajili ya kuhujumu timu.
“Nawapongeza wote kwa ujumla wenu kwa heshma hii mliyowapa wachezaji kwani naamini itakuwa chachu katika kuendeleza mchezo wa soka nchini,” alisema Nyamlani.


Comments