WAREMBO 11 WAJITOSA MISS KIGAMBONI 2013
WAREMBO 11 kutoka sehemu mbalimbali wamejitokeza kushiriki shindano la kumsaka malkia wa kitongoji cha Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" linalotarajiwa kufanyika Ijumaa Juni 7 kwenye ukumbi wa Navy Beach kuanzia saa 2:00 usiku hapa jijini Dar es Salaam.
Tayari warembo wameshaanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na shindano hilo ambapo wanajifua kwenye ukumbi wa Break Point (VIP) uliopo Posta hapa jijini.
Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu (pichani), alisema kuwa maandalizi ya shindano hilo yako katika hatua za mwisho na bado wanakaribisha warembo wenye sifa za kushiriki shindano hilo kufika mazoezini kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
Aliwataja warembo ambao wameshaanza mazoezi kuwa ni pamoja na Rogathe Michael, Irene Rajab, Magdalena Olotu, Latifa Mohammed, Axsaritha Vedastus, Angella Lutataza, Sara Makembo, Amina Mussa,  Ellen Sulle, Julieth Mwanri na Rachel Reuben.
"Tunatarajia kuwa na shindano lenye mvuto na litakalotoa washindani kwenye mashindano ya kanda na baadaye katika ngazi ya taifa, tumejipanga kufanya mapinduzi ndani ya sanaa hii ya urembo wa hapa nchini," alisema Somoe.
Aliongeza kwamba fomu kwa ajili ya kushiriki shindano hilo zinapatikana bure na warembo wanafanya mazoezi chini ya Blessing Ngowi, ambaye mwaka juzi alishiriki fainali za taifa za Redd's Miss Tanzania na alitwaa taji la Kanda ya Elimu ya Juu.
Aliyataka makampuni na taasisi mbalimbali zinakaribishwa kudhamini shindano hilo ambalo mwaka jana lilitoa mshindi katika kinyang'anyiro cha Kanda ya Temeke ambaye ni Edda Sylivester.
Wadhamini ambao wamethibitisha kusaidia shindano hilo ni pamoja na kampuni ya bia Tanzania kupitia kinywaji cha Redd's Premium Original, Montage Limited, Clouds Media Group, Papa Z na Break Point.
Taji la Redd's Miss Tanzania linashikiliwa na Brigitte Alfred wakati Edda alishika alifanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye fainali hizo za taifa mwaka jana.