SIMBA YATAKATA MWANA WAKE...YANGA WAJIPANGE

Mfungaji wa bao la Simba, Haroun Chanongo, wa pili kutoka kushoto akishangilia na Ramadhani Singano 'Messi'. Kulia ni wachezaji wenzake wakimpongeza. 


Na Mahmoud Zubeiry, MEI 8, 2013
SIMBA SC imefufua matumaini ya kucheza michuano ya Afrika mwakani, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Mgambo jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Andrew Shamba, aliyesaidiwa na Abdallah Rashid na Abdallah Mkomwa wote kutoka Pwani, hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na kiungo hatari wa pembeni, Haroun Athumani Chanongo dakika ya nane, ambaye aliombea mpira katikati ya Uwanja na kuanza kuwapangua mabeki wa Mgambo kabla ya kumchambua kipa Godson Mmasa.
Baada ya bao hilo, Simba SC waliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Mgambo na Amri Kiemba alikaribia kufunga mara mbili wakati Nassor Masoud ‘Chollo’ na Ramadhani Singano ‘Messi’ kila mmoja alikaribia kufunga mara moja.
Kipindi cha pili, Mgambo JKT walipambana kutoruhusu mabao zaidi, ingawa Simba SC iliendelea kutawala mchezo huo kwa pasi maridadi na soka ya kuvutia.
Katika mchezo huo, kipa Juma Kaseja aliokoa hatari mbili tu kipindi cha kwanza moja alipopangua shuti la juu kabla ya kudaka na kipindi cha pili alipodaka shuti la chini, pembeni.
Ushindi huo, unaifanya Simba SC itimize pointi 45, sasa ikizidiwa tatu na Azam FC inayoshika nafasi ya pili, ambayo Jumapili itamenyana na Mgambo kwenye Uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi.  
Katika mchezo wa leo, kocha Mfaransa Patrick Liewig aliwapumzisha wachezaji kadhaa tegemeo, Mrisho Ngassa, Shomary Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu na Mussa Mudde kuelekea mchezo dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga Mei 18.   
Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’/Omary Salum, Haruna Shamte, Miraj Adam, Hassan Khatib, Jonas Mkude, Edward Christopher, William Lucian ‘Gallas’/Rashid Ismail, Amri Kiemba, Ramadhani Singano ‘Messi’/Salim Kinje na Haroun Chanongo.
JKT Mgambo; Godson Mmasa, Salum Mlima, Ramadhani Kambwili, Bashiru Chanacha, Bakari Mtama, Salum Kipanga, Chande Magoja/Mussa Gunda, Peter Mwalyanzi, Issa Kandulu, Fully Maganga na Nassor Gumbo. 

TATU BORA LIGI KUU YA VODACOM:   
                   P W D L GF GA GD Pts
1 Yanga SC 25 17 6 2 45 14 31 57
2 Azam FC  24 14 6 4 42 20 22 48
3 Simba SC 25 12 9 4 38 23 15 45

Comments