ALIYEKUWA kiungo wa Simba,
Haruna Moshi ‘Boban’ anatarajiwa
kutimkia Doha, Qatar kwa ajili ya kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu
moja inayoshiriki ligi daraja la pili nchini humo.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam juzi, mdau anayeshughulikia safari hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina
lake alisema kwamba tayari wameshatuma hati ya kusafiria ya mchezaji huyo
nchini Qatar kwa ajili ya kupatiwa kibali cha kuingia nchini humo (viza).
Alisema kwa asilimia kubwa
safari ya mchezaji huyo imeiva na anatarajiwa kuondoka wakati wowote kuanzia
sasa pindi viza hiyo itakaporejeshwa nchini.
Aliongeza kuwa, kabla ya
kusajiliwa mchezaji huyo kwanza atafanya majaribio kwa wiki kadhaa ili uongozi
uweze kujiridhisha zaidi na kiwango chake.
Iwapo nyota huyo atafanikiwa
kusajiliwa na klabu hiyo itakuwa ni mara yake ya pili kwenda kucheza soka la
kulipwa ambapo miaka ya nyuma alipata kusajiliwa na klabu ya Gefle IF ya nchini
Sweeden kabla ya kuvunja nayo mkataba.
Aidha, Boban ambaye amekuwa
akitumika ndani ya klabu ya Simba kwa miaka kadhaa, kabla ua kumalizika kwa
msimu uliopita wa ligi kuu bara alisimamishwa kwa muda usiojulikana kuitumikia
klabu hiyo kutokana na utovu wa nidhamu yeye pamoja na beki, Juma Nyoso.
Tayari uongozi wa Simba
umetangaza kutomsajili tena Boban aliyemaliza mkataba wake.
Katika hatua nyingine, kikosi
cha Simba kilianza rasmi mazoezi jana chini ya kocha wake mpya Abdallah ‘King’
Kibadeni, amzoezi yaliyofanyika kwenye uwanja wa Kinesi jijini Dar es Salaam.
Simba inatarajiwa kushiriki
michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame
inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 18 hadi Julai 2 nchini Sudan ambapo leo
kitaendelea na mazoezi yake asubuhi na jioni.
Comments
Post a Comment