YANGA YAKABWA KOO NA MGAMBO LEO MKWAKWANI

Simon Msuva akiwa nyavuni na mpira, baada ya kufunga huku Nurdin Bakari na Nizar Khalfan wakishangilia


Na Mahmoud Zubeiry, Tanga
BAO la kiungo wa pembeni, Simon Msuva katika dakika ya 86, jioni hii limeinusuru klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam kuzama mbele ya Mgambo Shooting ya Handeni, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga baada ya kulazimisha sare ya 1-1.
Sare hiyo inamaanisha mbio za ubingwa bado zinaendelea kati ya Yanga SC yenye pointi 53 kileleni sasa na Azam FC yenye pointi 47.
Hadi mapumziko, Mgambo walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Issa Kanduru aliyemgeuza kwenye eneo la hatari beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kabla ya kumtungua Ally Mustafa ‘Barthez’, baada ya kupokea pasi nzuri ya Salum Mlima.
Mgambo walitawala sehemu kubwa ya mchezo wa kipindi cha kwanza na kupeleka mashambulizi mengi zaidi langoni mwa Yanga, ambayo zaidi walikuwa wakipiga mirefu kwa lengo la kushambulia moja kwa moja.
Mchezo pia ulikuwa wa ‘kibabe’ na dakika 45 za kwanza zilimalizika kiungo Frank Domayo akiwa ana ngeu jicho la kushoto baada ya kupigwa kisukusuku na mchezaji mmoja wa Mgambo.
Dakika 44 zilitosha kwa Hamizi Kiiza katika mchezo wa leo, baada ya kugongwa na beki mmoja wa Mgambo na kushindwa kuendelea na mchezo, akimpisha Said Bahanuzi.
Kipindi cha pili, Yanga SC ilianza na mabadiliko, ikiwatoa Domayo aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nurdin Bakari na baadaye Oscar Joshua akampisha Haruna Niyonzima.
Mabadililo hayo yaliongeza uhai katika Yanga SC na kuanza kulishambulia lango la Mgambo JKT mfululizo hatimaye dakika ya 86, Msuva aliambaa upande wa kulia wa uwanja, akiwatoka mabeki wa Mgambo na kufanya kama anataka kutoa pasi, akaingiza mpira nyavuni moja kwa moja.
Msuva hakutaka hata kushangilia bao hilo zaidi ya kwenda kuuwahi mpira kwenye nyavu za Mgambo ili akauweke kati na alilazimika kugombea mpira na beki wa timu hiyo, ambaye alitaka uendelee kubaki ili kupoteza muda. 
Katika mchezo huo, kikosi cha Mgambo JKT kilikuwa; Godson Mmasi, Salum Mlima, Juma Roisana/Yassin Awadh, Bashiru Chanacha, Bakari Mtama, Salum Kipanga, Chande Magoja/Omar Matwiko, Mussa Mgunda, Issa Kanduru, Fulla Maganga na Nassor Gumbo.
Yanga SC; Ally Mustafa, Mbuyu Twite, Oscar Joshua/Haruna Niyonzima, Nadir Haroub, Kevin Yondan, Athumani Iddi, Frank Domayo/Nurdin Bakari, Hamisi Kiiza/Said Bahanuzi dk44, Nizar Khalfan na David Luhende. 

Comments