Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya bao jioni ya leo
VINARA wa ligi kuu ya Vodacom , Yanga Sc leo wameendelea
kujiwekea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuwachapa mabao
3-0 maafande wa JKT Oljoro katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa kwenye uwanja
wa Taifa.
Ushindi huo umeivua rasmi ubingwa Simba kwani Yanga
imefikisha pointi 52 huku ikisaliwa na mechi tatu ambapo kama itashinda itafikisha pointi 61 huku Simba inayoshika nafasi ya nne ikiwa
na pointi 35 hata kama ikishinda mechi zake tatu zilizosalia itafikisha pointi
44 tu.
Kwa mantiki hiyo sasa mbio za ubingwa wa Ligi hiyo utawaniwa
na Yanga pamoja na Azam Fc ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 46 na
kusaliwa na mechi nne ambapo ikishinda
zote itafikisha pointi 52,lakini ubingwa wa Azam utategemea kama Yanga
itapoteza mechi zake zilizosalia.
Katika mchezo wa leo, iliwachukua dakika ya tano Yanga kupata
bao lao la kwanza kupitia kwa Nadir
Haroub ‘Canavaro’ aliyefunga kwa kichwa
akiunganisha kona ya Athuman Idd ‘Chuji’.Kona
hiyo ilikuja baada ya kipa wa Oljoro kufanya kazi ya ziada kupangua shuti kali
la Simon Msuva.
Dakika mbili baadaye, Hamis Kiiza alishindwa kuifungia Yanga
bao akiwa na kipa baada ya kupokea pasi ya Simon Msuva aliyekuwa mwiba kwa walinzi
wa Oljoro.
Dakika ya 19, Msuva aliipatia Yanga bao la pili kwa shuti la
nje ya boksi baada ya kumlamba chenga beki wa Oljoro na jitihada za kipa wa
Oljoro Lucheke Musa kuokoa shuti hilo
hazikuzaa matunda.
Didier Kavumbagu aliikosesha Yanga bao jingine katika dakika
ya 24 baada ya kushindwa kuitendea hali
krosi ya Msuva, kabla ya dakika ya 32, beki wa Yanga Juma Abdul kuumia baada ya
kugongana na winga wa Oljoro.
Dakika ya 36, Msuva alikosa bao baada ya shuti lake kutoka
sentimiuta chache kwa juu, huku Yanga ikiutawala zaidi mchezo huo.
Hamis Kiiza aliipatia Yanga bao la tatu katika dakika ya 43
akitumia mpira mrefu kumzidi ujanja kipa wa Oljoro aliyetokea bila mafanikio.Hadi
timu hizo zinakwenda mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu kucheza mpira wa
kutegeana kabla ya Oljoro kuanza kucheza rafu zisizo za msingi ambapo dakika ya
56, Emmanuel Memba alipewa kadi ya jnjano baada ya kumchezea rafu Kiungo wa
Yanga, Haruna Niyonzima
Dakika ya 60 nyota wa kimataifa wa Yanga, Didier Kavumbagu
aliumia na kushindwa kuendelea ambapo nafasi yake ilichulkuliwa na Said Bahanuzi
Katika mchezo huo pia, mchezaji wa Oljoro Majaliwa Sadik
alizawadiwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Msuva
Dakika ya 87 kipa wa Oljoro alifanya kazi ya ziada kupoangua
shuti la mbali la Nizar Khalfanm na kuwa kona tasa, kabla ya dakika tatu
baadaye Bahanuzi kukosa bao la wazi baada ya kipa wa Oljoro kutokea na kupaisha
juu.
Katika mchezo wa jana, Yanga iliwatoa Juma Abdul, Kavumbagu
na Msuva na kuwaingiza Shadrack
Nsajigwa, Bahanuzi na Nizar Khalfan huku Oljoro ikiwatoa Kipa LKucheke, Karage
Mgunda na kuwaingiza Shaibu Issa na Sixbert Mohammed.
Yanga: Ali Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, David Luhende,
Nadir Haroub ‘Canavaro’,Kelvi Yondan, Athuman Iddi ‘Chuji’,Simon Msuva, Frank
Domayo, Didier Kavumbagu na Haruna
Niyonzima.
Oljoro:Lucheke Musa, Yusuph Machogoti, Majaliwa Sadiki,
Nurdin Mohamed, Shaibu Nayopa, Salim Mbonde, Karage Mgunda, Emmanuel Memba,
Paul Nonga, Idd Swaleh na Hamis Saleh.
Comments
Post a Comment