SIMBA YAKUBALI YASRE NA AZAM FC, YALIA NA MWAMUZI


PAMOJA na kukubaliana na matokeo ya mechi ya jana dhidi ya Azam, uongozi wa Simba unapenda kuweka rekodi wazi kwamba haukuridhishwa na uchezeshaji wa mwamuzi, Oden Mbaga (pichani), hasahasa katika kipindi cha pili.
Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, kwa bahati nzuri, msimamo huu wa Simba hauna hata chembe ya ushabiki kwa vile hata washabiki waliokuwa katika upande wa watani wetu wa jadi, nao pia walionekana kutofurahishwa na uchezeshaji wa Mbaga.
Mbaga ni mwamuzi mwenye beji ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na katika hali ya kawaida ilitazamiwa mechi ingechezeshwa kwa viwango vya kimataifa lakini hali ilikuwa kinyume chake.
Simba inaamini kwamba Mbaga hakuutendea haki mchezo ule wa jana. Simba inasema hivi kwa sababu inataka mwamuzi huyo ajirekebishe na kwamba matokeo ya mechi viwanjani yaamuliwe na ubora wa timu na si maamuzi yenye utata.