SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), linatarajiwa
kumlima barua ya onyo Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga(pichani),
imefahamika.
Hatua hiyo inatokana na Sanga kudai kwamba TFF
inataka kuihujumu klabu hiyo, baada ya kusogeza mbele mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi
ya JKT Oljoro uliokuwa ufanyike juzi hadi kesho.
Shirikisho hilo lilifanya mabadiliko ya mchezo
huo na ule wa Simba na Azam FC uliokuwa upigwe kesho kwenye Uwanja wa Taifa,
ambao sasa utapigwa kesho kutwa, ili kutoa nafasi kwa mechi hizo kuoneshwa ‘live’
na kituo cha televisheni cha Super Sport.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu
Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kwamba kauli ya Sanga ni upotoshaji mkubwa,
kwani shirikisho hilo halipo katika kuhujumu timu yoyote, bali kuzisaidia klabu.
Alisema mechi kuoneshwa ‘live’ na kituo kikubwa
kama Super Sport, inasaidia mambo mengi, ikiwamo kuzipa uzoefu wa kimataifa
timu husika, pia kutoa fursa kwa wachezaji kuonekana katika nchi tofauti.
Yanga ambayo inaongoza ligi hiyo kwa pointi 49,
ilitishia kutopeleka timu uwanjani baada ya mabadiliko hayo ya ratiba, kabla ya
juzi kusalimu amri na kukubali kuingiza timu uwanjani.
Comments
Post a Comment