BODABODA YASABABISHA KIFO CHA MCHEZAJI POLISI TABORA


Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mshambuliaji wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ya Polisi Tabora, Regan Mbuta kilichotokea jana (Machi 31 mwaka huu) usiku kwa ajali ya pikipiki mjini Tabora. 
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA), Yusuf Kitumbo, marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo (Aprili 1 mwaka huu) kwenda kijijini kwao Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko. 
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mbuta alikuwa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa Polisi Tabora, na bao lake la mwisho aliyoifungia timu ilikuwa kwenye mechi ya mwisho ya FDL msimu huu dhidi ya Pamba ya Mwanza iliyochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora. Hivyo mchango wake tutaukumbuka daima. 
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mbuta, TAREFA na klabu ya Polisi Tabora na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Mbuta mahali pema peponi. Amina