TFF YADAIWA KUTAKA KUPOTOSHA UMMA KUHUSU WARAKA WA FIFA


Rutayuga kulia akiwa na Jamal Malinzi kushoto, Mwenyekiti wa KRFA


Na Mahmoud Zubeiry
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoka Chama cha Soka Kagera (KRFA), Pelegrinius Rutayuga amesema TFF inataka kuupotosha tena umma kuhusu mchakato wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kubadilisha Katiba yake. 
Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Rutayuga amesema kwamba katika kile kinachoitwa taratibu za marekebisho ya Katiba yake, FIFA iliunda kikosi kazi kufanya mchakako wa awali wa mabadiliko hayo.
Rutayuga, aliyekuwa Meneja wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ambayo ilifuzu kucheza Fainali za Afrika mwaka 2005, lakini ikatolewa kwa kumtumia Nurdin Bakari aliyezidi umri, alisema katika mchakato huo kuna mambo 10 yanayotakiwa kubadilishwa.
Amesema katika kutekeleza mpango huo, FIFA imeandaa taratibu kadhaa, ili kufanikisha zoezi hilo, lakini chombo cha mwisho kitakuwa ni Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo.
Amesema FIFA ilianza na kutuma waraka wa kwa nchi wanachama wake wote, Oktoba 5, mwaka jana, ili kutoa mapendekezo yao juu ya mambo hayo 10 yanayotakiwa kubadilishwa.
“Ndiyo huu sasa waraka ambao TFF, wamekaa nao tangu Oktoba mwaka jana, lakini wanakuja kuutangaza leo, baada ya kuona Serikali imepinga mabadiliko yao ya Katiba kwa njia ya waraka, lengo hapa ni kutaka kuuhadaa umma,”alisema Rutayuga.
Amesema baada ya kupokea mapendekezo kutoka vyama vya soka vya nchi wanachama wake, kutakuwa na kikao Februari 26, mwaka huu kitakachohusisha Makatibu wote wa mashirikisho ya Mabara pamoja na watalaamu wa sheria kutoka katika mashirikisho hayo, kikiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FIFA, Theo Zwanzinger kupitia mapendekezo ya kikosi kazi na kuandaa ripoti.
Alisema baada ya hapo, kutakuwa na kikao kingine, Machi 7, mwaka huu cha Kamati ya Sheria ya FIFA, ili kutengeneza rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba, ambayo itapelekwa kwenye Kamati ya Utendaji ya shiriksiho hilo.
Ameongeza kuwa, Kikao cha Kamati ya Utendaji ya FIFA kupitia na kupitisha rasimu hiyo, ili iwasilishwe kwenye Mkutano Mkuu wa bodi hiyo ya soka duniani, kitafuatia Machi 20 na 21, mwaka huu.  
Ruta amesema kwamba baada ya hapo, ndipo FIFA itafanya Mkutano Mkuu Mei 31, mwaka huu nchini Mauritius, ili Wajumbe wapitie na kupigia kura mabadiliko hayo.
“Maamuzi ya mwisho ya kupitia mabadiliko hayo yatafanywa ndani ya Mkutano Mkuu wa FIFA kule Mauritius, tarehe thelathini na moja mwezi wa tano mwaka elfu mbili na kumi na tatu, hawa jamaa wasitake kuupotosha umma bwana,”alisema Rutayuga.
Maelezo haya ya Rutayuga, yanafuatia taarifa ya TFF leo kwamba, FIFA, limetuma mapendekezo 10 ya marekebisho ya Katiba yake kwa wanachama wake kwa njia ya waraka.
Taarifa ya TFF imesema kwamba, mapendekezo hayo yametumwa kwa kila nchi mwanachama kupitia waraka namba 1320, ambapo wanachama kwa kupitia kwa mashirikisho yao ya mabara watapiga kura ya ndiyo au hapa. 
Kwa upande wa Afrika, wanachama wa FIFA wanatakiwa kuwasilisha kura zao kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Baadhi ya mapendekezo hayo ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa FIFA (FIFA Congress). 
Makamu wa Rais wa FIFA na wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaochaguliwa katika mabara ambapo itabidi wathibitishwe na FIFA Congress.
Muundo wa Kamati ya Utendaji; nafasi moja ya vyama vya mpira wa miguu vya Uingereza (British FAs) sasa inahamishiwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA). 
Pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya FIFA anatakiwa kushiriki vikao vya Kamati ya Utendaji bila kuwa na haki ya kupiga kura.
Uchaguzi wa Rais; mgombea anatakiwa kuungwa mkono na idadi ya kutosha ya vyama wanachama kutoka katika mabara mawili tofauti. Ukomo wa uongozi; kuanzisha vipindi vya uongozi. Ukomo wa umri; ukomo wa umri usiozidi miaka 72 wakati wa kugombea utekelezwe.
Uwakilishi wa kutosha kwa makundi yenye maslahi katika FIFA; makundi yenye maslahi katika mpira wa miguu kama wachezaji wapate uwakilishi katika Kamati ya Mpira wa Miguu. Uteuzi wa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia; uteuzi sasa ufanywe na Mkutano Mkuu wa TFF.
TFF iko njia panda kwa sasa, kufuatia serikali kuizuia kutumia Katiba mpya ya mwaka jana, kwa kuwa haikufuata taratibu za Kikatiba katika kuipitisha.
Zuio la kutumia Katiba mpya, limekuja wakati ambao TFF ipo katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu, ambao ulipangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.
Lakini kabla ya serikali kuzuia utumiwaji wa Katiba mpya, tayari FIFA ilikwishasitisha uchaguzi huo, kufuatia baadhi ya wagombea walioenguliwa kwenda kulalamika katika bodi hiyo, ili waje kuchunguza sakata la kuenguliwa kwao.
Baada ya kupokea agizo la serikali kuzuiwa kutumia Katiba mpya, Kamati ya Utendaji ya TFF ikapanga kukutana kesho ili kujadili agizo hilo

Comments