NYOTA WAKONGWE SIMBA SC 'WANUKA'


KUFUNGASHWA virago kwa timu ya Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kumeweka kwenye wakati mgumu wachezaji wakongwe wa timu hiyo, imefahamika.
Juzi, Simba iliaga michuano hiyo katika hatua ya awali baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0; ilinyukwa 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa wiki mbili zilizopita kabla ya kulimwa 4-0 waliporudiana
mjini Libolo.
Habari kutoka ndani ya klabu ya Simba, zinasema uongozi umedhamiria kuwaondoa wakongwe hao kundini kwani ndio chachu ya timu kupata matokeo yasiyoridhisha katika michezo yake ya hivi karibuni.
Katika kikao cha dharula cha kamati ya utendaji ya Simba wiki iliyopita kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili mwenendo mbovu wa timu hiyo katika siku za hivi karibuni, ilibainika wakongwe ni moja ya sababu.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa, wakongwe hao wamekuwa wakieneza ‘virusi’ vibaya kwa chipukizi, hivyo kuathiri ufanisi wa timu hiyo dimbani, hivyo uongozi unakuzudia kuchukua uamuzi mgumu kwa maslahi ya timu hiyo.
Kilisema kutokana na uongozi kuchoshwa na hali hiyo, umeona ni heri kuwaondoa kundini watovu wote wa nidhamu ili kutoa nafasi yaw engine kusajiliwa ambao watashirikiana na wengine wenye nidhamu waliopo kwenye timu hiyo na kusema katika hilo hawatajali umaarufu wa mchezaji.
 “Hatutaaangalia sura, uzoefu wala kiwango, tutawafyeka wote wanaoleta haya matatizo na uamuzi huo tutaanza kuutekeleza hivi karibuni,” alisema kiongozi huo bila kutaja wachezaji wanaodaiwa kueneza virusi katika timu hiyo.
Hata hivyo, baada ya kikao hicho ambapo pamoja na mambo mengine kiliazimia kuitisha mkutano mkuu wa dharula wa wanachama, wachezaji kwa upande wao walikutana  na kamati ya ufundi na kueleza wamekuwa wakikwazwa na mmoja ya makocha na baadhi ya viongozi.
Wacheza walikwenda mbali na kufichua kufanya vibaya kwa timu hiyo, si bahati mbaya isipokuwa kufikisha ujumbe wa kuwakataa kocha huyo na baadhi ya viongozi kwa kuwapendelea baadhi ya wachezaji wakati wachezaji wote wanapaswa kupewa haki sawa ndani ya timu.
Mbali ya kung’olewa kwenye michuano ya kimataifa, Simba pia imekuwa na mwendo mbaya kwenye kampeni za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 31, ikitanguliwa na kinara Yanga yenye pointi 42 na Azam ya pili kwa pointi 36.
Novemba mwaka jana, uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake Ismail Aden Rage, ulimtimua aliyekuwa kocha mkuu Mserbia, Milovan Cirkovic kwa kile kilichoelezwa kufanya vibaya kwa timu hiyo baada ya kumaliza raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ikiwa nafasi ya tatu.
Nafasi yake ikazibwa na Mfaransa Patrick Liewig, akisadiwa na Jamhuri Kihwelo huku kocha wa makipa akiwa James Kisaka na Meneja ni Mosea Basena.

Comments