MFALME WA TEMEKE KUJULIKANA KESHO@DAR LIVEHatimaye ile siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu imewadia wakati makundi mawili hasimu ya TMK Wanaume Halisi na TMK Wanaume Family yatapochuana kesho katika jukwaa la Dar Live ili kutafuta ufalme wa Wilaya ya Temeke.

Kwa mujibu wa mratibu wa mpambano huo utakaofanyika katika ukumbi huo wa kisasa uliyopo Mbagala Zakhem jijini Dar, Luqman Maloto, makundi hayo pinzani yataumana jukwaani kwa awamu mbili tofauti na majaji watakusanya maoni yao kisha kumtangaza mshindi.
Majaji wa mpambano huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa burudani jijini Dar es salaam, wanatarajiwa kuwa prodyuza mahiri nchini P.Funky ‘majani’, DJ maarufu DJ Jaydee na Master Jay ambaye amejipatia sifa nyingi katika shindano la Bongo Star Search.

“Watashindana kwa awamu mbili, litaanza kundi la kwanza na kufuatiwa na la pili kisha kutakuwa na mapumziko mafupi kabla hawajarudi tena jukwaani kwa mzunguko wa pili na baada ya hapo matakokeo yatatangazwa,” alisema Maloto na kuongeza:
“Watakuwepo majaji hao ambao watajaji kwa kuangalia vigezo vya; mavazi (atakayependeza zaidi), kutawala jukwaa (stage performance), mwitikio wa mashabiki (kuwaimbisha).

“Nidhamu kwa mashabiki (kutofanya fujo), ujumbe wa nyimbo (message), free style (michano ya papo kwa papo) lakini hatutaruhusu lugha ya matusi.”
Kuhusu wakati wa mapumziko kwenye mpambano huo, Maloto amesema utakuwa ndiyo muda muafaka kwa mkali Prof. Jay pamoja na Malkia wa Mipasho Bongo, Khadija Kopa kutumbuiza, bila kumsahau Mfalme wa Taarab nchini, Mzee Yusuf ambaye atakuwepo kuanzia saa 10 jioni.
Shoo hiyo ipo chini ya udhamini wa bia ya Serengeti Premium Lager, Vodacom na kinywaji cha Pepsi.