JULIO AWAKINGIA KIFUA WACHEZAJI SIMBA SC


KOCHA Msaidizi wa timu ya Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amedai kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kulitokana na maandalizi hafifu na wachezaji hawapaswi kutupiwa lawama.
Mabingwa hao wa Tanzania, walijikuta wakitolewa kwenye michuano hiyo na Recreativo do Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0. Awali ilifungwa bao 1-0 nyumbani kabla ya kutandikwa 4-0 ugenini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Julio alisema timu yake haikupata maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kushiriki michuano ya kimataifa, tofauti na wenzao ambao waliipa umuhimu mkubwa michuano hiyo.
Alisema, hali hiyo ndiyo ilisababisha kikosi chake kuondolewa katika raundi ya kwanza tu, kitu ambacho ni cha kusikitisha na kutia uchungu kwa timu kubwa kama Simba.
Julio aliongeza kuwa kutokana na matokeo hayo, hakuna haja ya kuwatupia lawama wachezaji, kwani walijitahidi kutimiza majukumu yao kwa kucheza kwa kiwango kinachostahili, lakini walizidiwa na wapinzani wao.
Alisema matokeo yameshakuwa hayo, hivyo kwa sasa hawana budi kuachana nayo na kuelekeza nguvu zao Ligi Kuu Bara ili kuweza kujiweka katika mazingira mazuri zaidi.
“Tutahakikisha tunafanya maandalizi ya hali ya juu ili tuweze kushinda michezo yetu iliyobaki na hivyo kupata nafasi nzuri itakayotuwezesha kushiriki michuano ya kimataifa mwakani,” alisema.
Simba kwa sasa inashika nafasi ya tatu ya ligi hiyo ikiwa na pointi  31 huku Azam FC ikiwa ya pili na pointi 36 na Yanga inayoshikilia usukani ina pointi 42.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Simba jana ulikuwa na kikao na wachezaji kwa ajili ya kujadili mustakabali wa timu yao, ambayo imekuwa na mwenendo mbaya katika mechi zake za hivi karibuni, zikiwemo za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Habari zilizopatikana jana jioni zinaeleza kwamba, Kamati ya Utendaji ya Simba, pamoja na viongozi wa Kamati ya Ufundi, walikutana na wachezaji baada ya mazoezi ya jioni na kujadili kiini cha kufanya kwao vibaya.
Kiongozi mmoja wa Simba, aliliambia Tanzania Daima kwamba, lengo la kikao hicho ni kubaini tatizo ili kulitatua na hatimaye kuondokana na mwenendo mbaya.
Hivi karibuni, kumekuwepo na ‘sintofahamu’ ndani ya klabu hiyo, ambapo kuna taarifa za mgomo wa chini chini unaofanywa na wachezaji kwa madai ya kubaguliwa na baadhi ya viongozi, huku pia wakilalamikia benchi la ufundi.

Comments