Skip to main content

AZIM DEWJI:NI BORA TZ IKAFUNGIWA KULIKO KUYUMBISHWA NA TENGA


Na Mwandishi Wetu
MWANAMICHEZO aliyewahi kuifadhili Simba na pia kumiliki timu ya Ligi Kuu ya soka nchini, Azim Dewji ameingilia katika suala la mgogoro wa Katiba ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), akisema ni bora Tanzania
ikafungiwa na FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kuliko
kuyumbishwa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Dewji aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, huku akimtaka Tenga kuwa na msimamo katika maamuzi yake.
Alisema kuwa, Tenga akiwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Michezo laTaifa (BMT) alikuwa tayari kuona Tanzania inafungiwa na FIFA, kulikokuacha soka la nchi hii liendeshwe kiholela.
“Sasa kama wakati ule alitaka tufungiwe, kwa sasa anaogopa nini na kuanza kubishana na Serikali?
“Kwa maoni yangu, ni bora tufungiwe lakini tusiendeshwe na
FIFA…Tanzania ina Serikali na ndiyo inayosimamia michezo, kwa hili sioni sababu ya TFF kuitunishia msuli serikali. Hii ni nchi, haiwezi kutishwa na taasisi tu ya soka ya kimataifa ambaye Tenga mwenyewe aliwahi kukaririwa miaka ya nyuma akisema ina genge la wahuni…,”
alisema Dewji.
TFF imejikuta ikiingia katika mgogoro na Serikali baada ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuingilia kati suala la mgogoro wa uchaguzi ndani ya TFF kwa kuagiza kufutwa kwa
matumizi ya Katiba ya shirikisho hilo ya mwaka 2012, kwa kuwa imekiuka Kanuni na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Waziri huyo aliiagiza TFF kufuata utaratibu wa kurekebisha Katiba za vyama vya michezo, kwa mujibu wa Sheria ya BMT iliyotungwa na Bunge pamoja na Kanuni zake ambazo ziko wazi na rahisi kuzifuata.
Hata hivyo uamuzi huo wa Waziri, ulipingwa na Tenga pamoja na Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, ambapo Tenga ameomba kuonana na Waziri akidai amepotoshwa na wasaidizi wake na uamuzi wake unaweza kulitia soka la Tanzania katika matatizo.
Tenga alidai Serikali na BMT vimeachana na kuingilia masuala ya soka tangu mwaka 2004 na ndani ya Katiba hiyo kuna utaratibu mzima ambao unaonesha namna ambavyo TFF inapaswa kufanya uamuzi wake kama chombo huru. Hata hivyo, kisheria Katiba ya TFF lazima isajiliwe serikalini.
Awali TFF iliomba kukutana na Waziri na ikafanya hivyo, lakini shirikisho hilo limeomba tena kukutana na Waziri Mukangara kwa madai kuwa katika kikao cha awali Tenga hakuwepo badala yake walienda watendaji, hivyo ni vyema kikafanyika kikao hicho ili kumpa ufafanuzi wa baadhi ya mambo kwa nia ya kulimaliza jambo hilo.
Katika kikao hicho cha awali, Serikali iliitaka TFF kuitisha mkutano wa katiba ndani ya siku 40 na baada ya hapo kuitisha uchaguzi ndani ya siku kama hizo na pia imeitaka kutoa taraifa kwa wanachama wake kuhusu mkutano huo ndani ya siku tano tangu siku walipokutana.
Uamuzi wa Dk  Mukangara ulikuja siku chache kabla ya timu ya maofisa wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuja nchini kufuatilia mgogoro ulioikumba TFF na wadau wake kutokana na masuala mbalimbali ya uchaguzi huo uliokuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu. Ujumbe wa FIFA
haukuja badala yake shirikisho hilo limetuma barua ya kutishia kuifungia Tanzania kama itathibitika serikali inaingilia masuala ya soka.