CHANZO cha kufanya vibaya kwa
klabu ya Simba kwenye michezo yake na
hasa Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea hivi sasa nchini ni mgomo baridi
unaondelea ndani ya kikosi cha timu hiyo, imefahamika.
Mabingwa hao watetezi wa ligi
hiyo wamejikuta wakipoteza ndoto zao za kutetea ubingwa wao baada ya kufanya
vibaya kwenye michezo yake ya ligi hiyo ambapo kwa sasa wanashika nafasi ya
tatu wakiwa na pointi 33 nyuma ya Azam Fc iliyo ya pili ikiwa na pointi 36 na
vinara Yanga wenye pointi 39.
Hali hiyo ilipelekea uongozi
wa Simba chini ya Mwenyekiti wake Alhaj Ismail Aden Rage kuitisha kikao chja
dharura mapema wiki hii ambapo moja ya maazimio yake ni kuitisha mkutano mkuu
wa dharura wa wanachama ili kujadili suala hilo.
Habari za kuaminika toka
ndani ya klabu hiyo zinaeleza kwamba mgomo huo baridi unatokana zaidi na
maslahi huku wakiwanyooshea vidole baadhi ya viongozi ambao wamekuwa chachu ya
mgawanyiko huo.
Immelezwa kuwa kuna baadhi ya
viongozi wamekuwa wakionesha upendeleo kwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo
hali ambayo si nzuri na hasa ikizingatiwa kuwa timu inaundwa na wachezaji wengi
na si baadhi.
“Unajua nini kwenye timu kuna
wachezaji zaidi ya 25 sasa iweje kiongozi au viongozi waoneshe kuwajali wachezaji
watano tu wakati kama shida na wengine pia wanashida, hii kitu haileti picha
nzuri ndiyo maana hata morali imeshuka,”kilieleza chanzo hicho.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa
ubaguzi huo wa kimaslahi unaofanywa na baadhi ya viongozi umekuwa ukiwaumiza
sana wachezaji hao na kujiona hawana faida ndani ya klabu hiyo na matokeo yake
kuamua kucheza bora liende tu.
Mbali na hilo, inadaiwa kuwa
maslahi na hasa mishahara ya
wachezaji haijaongezwa kwa muda mrefu
licha ya gharama za maisha kupanda kwa kasi sana kila kukicha.
“Kuna wachezaji wanafamilia
zinazowategemea, unampa mshahara huohuo kwa zaidi ya miaka mitatu unategemea
nini wakati yeye maisha yake yanategemea kucheza mpira tu,”kilidai chanzo
hicho.
Kwa upande mwingine inadaiwa
kuwa wachezaji hao wanachanganywa na uwepo wa makocha wengi ndani ya timu kitu
ambacho kinawafanya washindwe kufuata mafundisho ya nani.Simba ina makocha
wanne, kocha mkuu Patrick Liewig, ambaye anasaidiwa na Jamhuri Kihwelo, Moses
Basena na James Kisaka.
Akijibu shutuma hizo, ofisa habari
wa Simba Ezekiel Kamwaga pamoja na alisema hizo ni sababu za kitoto sana
kinachotakiwa ni kila mtu kutimiza jukumu lake lililompeleka kwenye klabu ya
Simba. “suala la mshahara kila mtu lipo ndani ya mkataba aliousaini, pia kuna
posho za kila siku kwenye mazoezi na mgawo wa mechi,”alisema
Kwa upande wa suala
kuchanganywa kutokana na uwepo wa makocha wanne, Kamwaga alisema halina mashiko kwani kila mtu
ana kazi yake ambapo kuna kocha mkuu (Liewig), msaidizi (Kihwelo), Meneja
(Basena) na Kocha wa makipa (Kisaka) na kudai kuwa wanaopaswa kuulizwa ni
viongozi wa kamati ya ufundi ambao wana jukumu la kuushauri uongozi kuhusiana
na masuala ya kiufundi.
“Vitu vingine vinashangaza
sana hebu ona klabu kama Manchester United ina makocha karibu 20 na mambo yako
vizuri, pia kila kocha yupo kwa kazi yake hivyo sidhani kama hili ni
tatizo,”aliongeza
Comments
Post a Comment