SIMBA WAMTANI MILOVAN, MWENYEWE ATAKA CHAKE KWANZA MENGINE YAFUATE


SIKU moja baada ya timu ya Simba kufungwa na Libolo ya Angola katika mechi ya kwanza hatua
ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, viongozi sasa wanatamani kumrejesha Mserbia Milovan Cirkovik (pichani kulia).
Habari zaidi zinasema hiyo haitokani na kufungwa bao 1-0 na Libolo tu, pia kushuka kwa kiwango cha timu hiyo hivyo kuambulia sare katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka
ndani ya uongozi wa klabu hiyo, tayari viongozi wameshamweleza Milovan kuhusu jambo hilo,
lakini ameweka ngumu akitaka kupewa chake kwanza.
Molovan kwa sasa yupo nchini akifuatilia stahili
zake zinazokadiriwa kufikia jumla ya dola 32, 000
za Marekani; karibia sh mil 50 za Tannzania.
Milovan aliyetupiwa virago baada ya kwisha kwa raundi ya kwanza Novemba mwaka jana, nafasi yake ilizibwa na Mfaransa, Patrick Liewig.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Milovan alikiri kuwa kwenye mazungumza na uongozi wa klabu hiyo wakitaka arudi, lakini anataka alipwe kwanza haki zake kabla ya mambo mapya.
“Kweli uongozi umekuwa na mazungumzo na
mimi ya kutaka kunirejesha kuinoa Simba, lakini nimewaambia wanilipe kwanza fedha zangu kabla ya kuketi kujadili hilo,” alisema.
Hata hivyo hakuna kiongozi wa Simba aliyepatikana jana kuzungumzia suala hilo, huku Ofisa habari wa timu hiyo Ezekiel Kamwaga simu yake iliita bila majibu.
Licha ya Simba kuwa chini ya jopo la makocha wanne wakiongozwa na Liewig, imekuwa na mwendo wa kusuasua kiasi cha mashabiki
kutaka kocha huyo arejeshwe.
Liewig amekuwa akisaidiwa na Mzambia Moses Basena, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Idd Pazi kwa upande wa makipa.
Aidha, yupo Talib Hilal aliyetua nchini kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi wakati timu hiyo ikijiandaa dhidi ya Libolo ya Angola.
Katika Ligi Kuu, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28, nyuma ya kinara Yanga yenye pointi 36 huku Azam ikiwa ya pili kwa pointi 33.