KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi
ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini
ya Mwenyekiti wake Idd
Mtiginjola, leo
ilitupa maombi ya kufanyia
marejeo (review) uamuzi wake kwa waombaji watano waliokuwa wamechujwa.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam jana, Mtiginjola alisema wamepitia Katiba ya TFF pia Kanuni za Uchaguzi
za TFF na kubaini hakuna Ibara inayotoa fursa ya review kwa uamuzi uliofanyika.
Alisema kwa mujibu wa Kanuni
za Mwenendo wa Madai (CPC) katika mahakama za kawaida, zinaruhusu Hakimu
aliyefanya uamuzi katika kesi kufanya marejeo, lakini katika masuala ya soka
hakuna fursa hiyo.
Kwa mazingira hayo,
Mtiginjola amesema kamati yake haiwezi kujitungia kitu kipya kwani kazi yao ni
kufanya uamuzi kwa kutafsiri Katiba na kanuni walizopewa
na mamlaka ya uteuzi, yaani TFF.
Waombaji watano waliokuwa
wakitaka Kamati hiyo ifanyie marejeo uamuzi wake kutupa rufani zao ni Jamal
Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa shirikisho hilo na wengine wanne.
Hao ni Hamad Yahya
aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu
(TPL Board).
Wengine ambao waliomba
kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano ni Eliud
Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha
Matutu (Shinyanga na Simiyu).
Baada ya kuchujwa, Malinzi
alimsihi Rais wa Shirikisho hilo, Leodegar Chilla Tenga kuingilia kati kutengua
uamuzi huo.
Hata hivyo, mwishoni mwa wiki
Tenga alisema hana uwezo huo, isipokuwa ni Kamati hiyo ya Rufaa kupitia upya
jambo hilo.
Alisema kama mgombea atakuwa
hajaridhika, bado anaweza kupeleka malalamiko yake Shirikisho la soka la
Kimataifa (Fifa) na wao TFF watampa ushirikiano wa kutosha.
Zaidi ya hapo, Tenga alisema
bado mgombea ana nafasi nyingine ya mwisho ya kuwasilisha malalamiko yake
Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (Cas).
Tenga alisema hivyo ndivyo
vyombo halali vinavyoweza kutoa haki na Shirikisho hilo likatoa ushirikiano kwa
mhusika katika kupigania haki anayodhani amepokwa.
Aidha, kutokana na kuwepo kwa
shinikizo la wagombea hao kutaka Kamati ya Mtiginjola kupitia upya uamuzi wake,
Kamati ya Uchaguzi chini ya Deogratius Lyatto ametangaza kusitisha mchakato wa
uchaguzi huo ambao ungefanyika Februari 24.
Kufanyika kwa uchaguzi huo ni
baada ya uongozi wa Tenga aliyekalia kwa mara
ya kwanza kiti hicho Desemba
27, 2004 kumaliza muda wake na hatakitetea tena.
Comments
Post a Comment