KIONGOZI SIMBA SC AAGA DUNIA


KLABU ya soka ya Simba inasikitika kutangaza kifo cha mjumbe wake wa Kamati ya Mashindano na Maendeleo ya Timu za Vijana, Hamis Mrisho maarufu kwa jila la Hamis Dalali aliyefariki dunia alfajiri ya leo kijijini kwake Matimbwa, Bagamoyo mkoa wa Pwani.
 
Mwenyekiti wa Simba, Alhaji Ismail Aden Rage, amesema msiba huo ni mzito sana kwa klabu na kwamba katika mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom, wachezaji na viongozi wa Simba watavaa vitambaa vyeusi kuashiria msiba huo mzito.
 
"Kwa niaba ya klabu ya soka ya Simba na kwa niaba yangu binafsi, naomba kutoa salamu zangu za rambirambi za dhati kabisa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kutokana na kifo cha ghafla ndugu Mrisho. Nilimfahamu kama mchapakazi wa kweli na mtu aliyeipenda Simba kwa moyo wake wote," alisema Rage.
 
Mrisho ambaye pia alikuwa Katibu wa Matawi ya Simba Wilaya ya Kinondoni, alikuwa ni mtu aliyekuwa akijituma sana kufanya kazi zozote za klabu kwa kadri ya maelekezo ya uongoz na hakuwa na makundi huku akipendwa na watu wote waliokuwa wakimfahamu.
 
Marehemu alizaliwa mwaka 1965 na ameacha mjane na watoto wanne. Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika leo jioni huko Matimbwa, Bagamoyo.
 
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, AMEN.
 
Imtolewa na
 
Ezekiel Kamwaga