YONO YAWABEBA YANGA VETERANS


Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Yamo, Stanley Kevela akizungumza na ujumbe wa Yanga Veterans (hawapo pichani) katika hafla ya kuwakabidhi vifaa vya michezo jijini Dar es Salaam jana. 

KAMPUNI ya Yono Action Mart ya jijini Dar es Salaam imeipiga tafu ya jezi timu ya Yanga Veterans ambayo inatarajiwa kushiriki Bonanza la wakongwe litakaloanza kutimua vumbi kwenye viwanja vya Sigara, Chang’ombe kesho.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi jezi hizo zenye thamani ya sh 600,000, Mwenyekiti wa Bodi, Yono Action Mart, Stanley Kevela, alisema, wameamua kutoa jezi hizo kwa kuheshimu na kutambua mchango wa nyota hao wa zamani katika klabu ya Yanga na Taifa kwa ujumla.
“Sisi Yono na Yanga ni marafiki na tuna bajeti yetu kabisa kwa ajili ya kusaidia mambo mbalimbali tunayoombwa na Yanga, kwani inapofanya vizuri inatufurahisha sana na hata kuimarisha ndoa zetu, maana ikifanya vibaya hata wake zetu tunawachukia. Hivyo tunaiombea Simba izidi kusuasua. Adui yako muombee njaa,” alisema Kevela na kuibua vicheko.
Kwa upande wake, nyota wa zamani wa yimu hiyo, ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako, aliipongeza kampuni ya Yono kwa ‘kupromoti’ michezo na si kwa Yanga tu, bali hata sehemu nyingine, na kuzitaka kampuni nyingine kuiga mrfano huo.
Naye Katibu wa Yanga Veterans, Mwanamtwa Kihwelo, kwa niaba yake, alishukuru msaada huo na kuwataka wadau wengine waige mfano huo wa kuwekeza katika michezo, wakiunga juhudi za Rais Jakaya Kikwete, kusaidia katika sekta hiyo.
“Tunamshukuru sana Yono, kwani amekuwa msaada mkubwa sana kwetu, si kwa msaada huu tu, bali haya mipango yetu mbalimbali ya kujikwamia kimaisha, ikiwamo uanzishaji wa Saccos,” alisema Kihwelo.
Naye beki mahiri, David Mwakalebela, alisema msaada aliyowapa Yono ni dawa, kwani kushiriki michezo na kufanya mazoezi kunaimarisha afya ya binadamu na kuepukana na maradhi mbalimbali.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na nyota wa zamani wa Yanga, ambako ukiacha Mwalusako, Mwanamtwa na Mwakalebela, pia alikuwepo Mohamed Hussein ‘Mmachinga’.
Bonanza hilo linaloshirikisha timu zilizokuwa zikitamba enzi za Ligi Daraja la Kwanza. Mbali na Yanga ambayo itafungua pazia na Pilsner, pia ziko Simba, Kariakoo Lindi, Coastal Union ya Tanga, Ushirika Moshi, Tukuyu Stars Mbeya, Pamba ya Mwanza, Bandari ya Mtwara na Reli ya Morogoro.


Comments