TFF YAIPONGZA AZAM FC KWA KUTWAA KOMBE LA MAPINDUZI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi wa klabu ya Azam kwa timu yao kufanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi mwaka huu. 
Kwa Azam kufanikiwa kutetea ubingwa huo inaonesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kabla ya kuingia katika mashindano hayo ambapo ilicheza fainali dhidi ya Tusker FC ya Kenya. 
Pia ushindi huo utakuwa changamoto kwa timu nyingine za Tanzania Bara zitakazopata fursa ya kushiriki michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi mwakani. Michuano hiyo iko kwenye Kalenda ya Matukio ya TFF.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA RUREFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Januari 10 mwaka huu.

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa RUREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Rukwa.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya RUREFA chini ya uenyekiti wa Blassy Kiondo aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Sumbawanga.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Rukwa kwa kuzingatia katiba ya RUREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Blassy Kiondo (Mwenyekiti), Gregory Seko (Katibu), John Maholani (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Ayoub Nyaulingo (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Gloria Ndawa (Mweka Hazina). Nafasi nyingine zitajazwa katika uchaguzi mdogo.


Comments