SIMBA YAIBANJUA LYON 3-1


MABINGWA wa ligi kuu ya Vodacom  Simba Sc leo wameuanza vema mzunguko wa pili baada ya kuitandika African Lyon mabao 3-1 katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba ambayo ilikwenda nchini Oman kuweka kambi maalum ya kujiandaa na Ligi hiyo, iliutawala mchezo huo jana zaidi sambamba na kutandaza kabumbu safi.
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ aliiandikia Simba bao la kwanza dakika ya pili akimalizia pasi ya Mrisho Ngassa,kabla ya Ngassa kuandika la pili katika dakika ya 18 baada ya kuwakimbiza mabeki huku akiwachambua na kumtungua kipa wa Lyon, Abdul Seif.
Katika mchezo huo, Jacob Massawe wa Lyon alikosa bao akiwa yeye na kipa Kaseja katika dakika  ya 5, huku Ngassa naye  akikosa mara mbili katika dakika ya saba na  14.Huku Massawe akikosa tena bao la wazi katika dakika ya  17 baada kuwashughulisha mabeki wa Simba na kukosa bao akiwa na kaseja.
Ngasa aliipatia Simba bao la tatu katika dakika ya 36 akiwa ndani ya boksi dogo akimalizia pasi ya Kiemba.
Wakati bao la kufutia machozi kwa Lyon lilifungwa katika dakika ya 60 mtokea benchi Bright Ike aliifungia Lyon akimalizia pande la Fred Lewis.

MATOKEO MENGINE:
AZAM v KAGERA SUGAR 3-1
RUVU SHOOTING v JKT RUVU 1-0
JKT OLJORO v TOTO AFRICAN 
POLISI MORO v MTIBWA SUGAR 1-0.
COASTAL UNION v MGAMBO SHOOTING 3-1