AZAM FC YAIFUKUZIA YANGA VPL


Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 15 kesho (Januari 30 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo Azam iliyo katika nafasi ya pili nyuma ya Yanga itakuwa mwenyeji wa Toto Africans ya Mwanza.

Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam huku Azam ikisaka ushindi ili kuikaribia Yanga inayoongoza wakati Toto Africans inayonolewa na John Tegete ikitaka kurekebisha makosa ya kupoteza mechi yake iliyopita dhidi ya Oljoro JKT.

Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT dhidi ya wageni Kagera Sugar kutoka Bukoba mkoani Kagera itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo wa Musoma.

Ushindi kwa Oljoro JKT yenye pointi 17 utaihakikishia kubaki katika nafasi yake ya nane wakati Kagera Sugar inayofundishwa na kocha mkongwe Abdallah Kibaden utaifanya ipige hatua moja mbele katika msimamo wa ligi.

Ligi itaendelea tena Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo vinara Yanga wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Polisi Morogoro ikiikaribisha African Lyon mjini Morogoro.

Nazo Mgambo Shooting ya Tanga na Ruvu Shooting ya Mlandizi mkoani Pwani zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.