ZANTEL YAMWAGA FEDHA SEMINA YA TASWA


Mkurugenzi wa Mahusiano wa Zantel, Ahmed Seif Mohamed (kushoto ), akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TASWA), Juma Abbas Pinto, mfano wa hundi ya thamani ya Sh. Milioni 6 na ushei, kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa chama hicho, utakaofanyika Desemba 21 na 22, mwaka huu Bagamoyo mkoani Pwani. Katikati ni Katibu Msaidizi wa TASWA, George John.


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zantel imejitokeza kudhamini Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) utakaofanyika Desemba 21 na 22 mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani Pwani.
A Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Zantel Ahmed Seif Mohamed, alisema wanajisikia furaha kushirikiana na TASWA kudhamini mkutano huo wa aina yake.
Alisema Zantel imekuwa na uhusiano mzuri na wanahabari, hivyo walipoombwa hawakusita kufanya hivyo na wana matumaini makubwa utakuwa mkutano wenye manufaa.
Alieleza kuwa kampuni yake baada ya kupata mafanikio katika mashindano ya Epiq Bongo Star Search iliyomalizika hivi karibuni ni nafasi nyingine ya kuendelea kudhamini matukio mbalimbali ya michezo na burudani kwa kadri uwezo utakavyoruhusu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru Zantel na kusema awali chama hicho kiliomba udhamini kwa kampuni hiyo kwa lengo la kufanya mkutano Dar es Salaam, lakini sasa walifikiria ufanyike Bagamoyo, Pwani.
Alisema Zantel wamedhamini kwa kiasi cha Sh 6,040,000 na kwamba bajeti ya mkutano huo ni Sh milioni 20, hivyo kuomba wadau wengine wasaidie ili kufanikisha mkutano huo utakaohusisha zaidi ya waandishi wa habari za michezo 100 ambao ni wanachama wa TASWA.
 “Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wanachama 100, na pia watakuwepo wadau mbalimbali wa TASWA wakiwemo waandishi wakongwe wa habari za michezo wambao watapewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo,” alisema Pinto.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho, aliwasisitiza wanachama kuendelea kuthibitisha ushiriki wao na kuwa mwisho wa kufanya hivyo ni kesho alasiri.

Comments