SIMBA SC WAJIVUNIA KOCHA WAO MPYA

Ezekiel Kamwaga, Ofisa Habari wa Simba

MABINGWA wa Soka Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam, wamejivunia kumpata kocha mpya, Mfaransa Patrick Liewig na kudai ataleta neema kubwa kwa timu hiyo kutokana na kufahamiana na makocha wengi ndani na nje ya Afrika.
Kocha huyo mwenye makazi yake nchini Ivory Coast, anatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam mara baada ya sikuu ya Krismas, akichukua nafasi ya Mserbia, Milovan Cirkovic ambaye ametupiwa virago kutokana na kutofanya vizuri kwa timu hiyo kwenye mbio za kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kwamba, ujio wa kocha
huyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kutimiza malengo ya timu hiyo, katika mpango wao wa kuendeleza vijana.
Alisema kutokana na uzoefu wa Liewig sambamba na kufanya kazi katika Academy za klabu kubwa chini ya makocha mahiri katika rekodi yake, wanaamini ujuzi na uzoefu huo sasa utahamia Msimbazi.
“Tunaamini sasa Simba itazalisha wachezaji wengi zaidi, ambao wataleta manufaa si kwa Simba tu, bali hata kwa timu nyingine za nje, kwani huyu mambo ya vijana ndio amekuwa nayo kwa miaka mingi,” alisema na kuongeza.
Pia huyu kocha anaweza kusaidia pia kuwawezesha wachezaji wetu kupata timu za kucheza nje, kwani ana ushirikiano na makocha wengi wa kubwa, wengine alishafanya nao kazi.
Kamwaga aliongeza kuwa, kutokana na kusogezwa siku za kuja kwa Kocha huyo, sasa wachezaji waliopo wataendelea na mazoezi ya viungo ‘Gym’, huku wengine waliopo timu ya Taifa wakiendelea kujinoa.
Liewing mwenye shahada ya ukocha, kabla ya kuja Simba alikuwa akifanya kazi katika klabu ya Club Africain ya Tunisia kama Mkurugenzi wa Ufundi, Meneja na pia meneja wa timu ya wachezaji wa kulipwa.
Pia amewahi kufanya kazi katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Misri, Brazil, Abu dhabi, Malaysia, Argentina, Ivory Coast na Tunisia.
Kwa upande mwingine, Simba imemshukuru kocha Milovan kutokana na kuiletea mafanikiwa, ikiwemo ubingwa wa ligi kuu bara msimu wa 2011/2012 na kuifikisha hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho, (CAF).

Comments