MOGELLA, MWAMEJA, MADARAKA NA PAWASA WAREJESHWA SIMBA SC

                                                                       Zamoyoni Mogela
                                                               Mohammed Mwameja

KATIKA kuhakikisha inafanya vema katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na michuano ya kimataifa, Simba imewarejesha nyota wake wa zamani wakiunda Kamati ya Ufundi ya timu hiyo.
Nyota hao waliojumuishwa katika kamati hiyo, chini ya mwenyekiti wake, Ibrahim Masoud ‘Maestro’, ni Zamoyoni Mogella, Madaraka Suleiman, Mohammed Mwameja na Boniface Pawasa.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, alitangaza kuvunja kamati zote kutokana na kushindwa kuleta ufanisi, ikimaliza raundi ya kwanza ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam FC.
Kamati zilizovunjwa ni Fedha, Mashindano, Ufundi, Usajili na Nidhamu, ingawa tayari alishamteua Zacharia Hanspoppe kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba, zinasema Rage amewateua Mogella,
Mwameja na Pawasa kutokana na uwezo na ushawishi kutokana na mchango wao kwa timu hiyo.
“Mwenyekiti ameona aingize na nyota wetu wa zamani ambao kila mmoja alikuwa anawakubali, hivyo kwa uwezo walionao kwa kiasi kikubwa watasaidia kwa namna moja ama nyingine mafanikio ya Simba.
“Hawa wamecheza ndani na nje ya nchi, pia wamekuwa karibu na soka hata baada ya kuachana na mchezo huu…nadhani watasaidia sana kuleta mabadiliko katika kikosi cha Simba,” kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Kiliongeza kwamba, kamati hiyo itakuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na benchi la ufundi, huku wachezaji wakianza mazoezi ya kujenga mwili ‘Gym’ wakimsubiri Kocha Mfaransa, Patrick Lieweing.
Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo ni Joseph Itang’are ‘Kinesi’, Sued Nkwabi ambao pia ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo na Said Tuliy.
Simba inakabiliwa na mitihani miwili; Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo itaanzia nyumbani dhidi ya CR Libolo ya Angola kati ya Februari 15 na 17, na kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu.