MIAKA 51 YA UHURU:JK AWATUNUKU BI KIDUDE, MAALIM GURUMO Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimtunuku  nishani ya  makundi mbalimbali yajamii waliotumikia taifa kwa uadilifu na kutoa mchango wa pekee Msanii Mkongwe Bi.Fatma Baraka Khamis(Bi.Kidude) Pichani juu.(picha na Freddy Maro).
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Bi Fatma Baraka Khamis,(Kidude) baada ya kutunukiwa nishani ya Sanaa na Michezo na Rais wa Tanzania Dk.Jakaya Mrisho Kikwete,(kulia) katika sherehe za kutunuku Nishani katika Viwanja vya Ikulu Dar es Salaam,(katikati)Rais Mstaafu wa Tanzania Mzee Mwinyi.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Na Abdallah Khamis 
MSANII mkongwe wa nyimbo za taarab nchini, Fatma Baraka Khamis ‘Bi Kidude’, jana aliwaacha watu hoi katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam, aliposhindwa kwenda kupokea nishani ya sanaa na michezo hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alipoacha kiti chake na kumfuata na kumvisha.
Tukio hilo lilitokea jana wakati Rais Kikwete alipokuwa akiwatunukia nishani watu mbalimbali kutokana na mchango walioutoa kwa ajili ya maendeleo ya taifa kitaifa na kimataifa, ambapo jumla ya wanamichezo watano walitunukiwa nishani hizo.
Wanamichezo wengine waliotunukiwa nishani hizo mbali na Bi Kidude ni pamoja na Muhidini Gurumo, mwanariadha mkongwe aliyejizolea sifa kitaifa na kimataifa, John Stephen Akhwari, pamoja na Marijani Rajab na Fundi Said ‘Mzee Kipara’ ambao wote ni marehemu.
Hali ya Bi Kidude kutaka afuatwe alipokaa ilianza kuonekana mapema wakati watu waliokuwa wakitarajia kutunukiwa nishani hiyo walipotajwa majina na kutakiwa kuinuka ambapo Bi Kidude hakuinuka wala kupunga mkono hatua iliyozua minong’ono kuwa huenda bado anaumwa.
Ilipofika wakati wa kwenda mbele kupokea nishani, Bi Kidude aliendelea kuonesha usanii wake kwa kuamua kuendelea kukaa kwenye kiti hadi alipofuatwa na kuvishwa nishani hiyo.
Wakati wa kwenda kupiga picha ya pamoja kwa watu waliotunukiwa, Bi. Kidude aliinuka huku akiongozana na Maalim Gurumo kwenda katika eneo lililopangwa kwa ajili ya picha hali ilyowaacha watu hoi kwa kicheko.
Katika hatua ya kushangaza, Bi. Kidude wakati akipongezwa na waandishi wa habari, badala ya kuwajibu aliinua mkuno hewani na kutanua vidole viwili kisha akapeleka mdomoni kama ishara ya mtu anayevuta sigara kisha akaondoka kwenda kukaa katika sehemu yake.