VODACOM YAIFAGILIA KILIMANJARO STARS


Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ambao ni wadhamini wakuu wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara imepongeza ushindi   na kiwango kilichoonyeshwa na Kilimanjaro Stars  dhidi ya Timu ya taifa ya Sudan jumapili iliyopita. 
Katika mchezo wake wa kwanza wa fainali za Cecafa zinazoshirikisha timu za taifa za nchi za Afrika Mashariki na Kati zinazofanyika nchini Uganda, Stars imeanza vema kwa kupata ushindi wa mabao 2-0. 
“Tunaipongeza Kilimanjaro Stars kwa ushindi huo kwani ni ushindi unaotoa matumaini ya kuendeleza rekodi ya mara kadhaa ya kufanya vema katika mashindano ya Cecafa.” Alisema Meza katika taarifa yake ya pongezi kupitia vyombo vya habari. 
Meza amesema kikosi bora cha timu ya taifa ni taswira nzuri ya ubora wa soka la ndani ikiwemo ligi kuu ambayo Vodacom imekuwa ikiidhamini na ambayo imeonesha kukua kiushindani na hivyo kuzalisha wachezaji imara kwa mashindano ya kimataifa.
Stars ipo kundi moja na Somalia, Burundi na Sudan na imeonyesha kandanda safi na la kuvutia na hatimaye kuvuna ushindi huo wa magoli mawili kupitia mshambuliaji wake John Boko anayechezea timu ya Azam FC. 
“Ni ushindi wa Watanzania wote na wadau wanaoitakia mema soka ya Tanzania, kwetu Vodacom ushindi huu unatupa nguvu, ari na chachu zaidi katika dhamira yetu ya dhati ya kukuza na kuendeleza mpira wa miguu nchini kwa faida ya washabiki, vilabu, wachezaji na taifa kwa ujumla.” 
Tanzania inawakilishwa pia na timu ya taifa ya Zanzibar – Zanzibar Heroes ambayo nayo pia imeonyesha kiwango kikubwa, Vodacom imaitakia pia kila la kheri katika mechi hiyo muhimu. 
Vodacom ndio mdhamini mkuu wa ligi kuu soka Tanzania Bara kwa zaidi ya miaka sita na hivyo kuwa moja ya wachangiaji wakuu wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini mchezo unaangoza kwa kuwa na idadi kubwa ya washabiki.