SIMBA SC WAENDA KUSAKA NYOTA CHALENJI



BAADHI ya wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, wanatarajiwa kwenda Kampala nchini Uganda kwa ajili ya kusaka nyota watakaowasajili kwa ajili ya kuziba mapengo ya wachezaji wake watatu wa kimataifa waliowatema hivi karibuni kutokana na kutoridhishwa na mchango wao dimbani.
Baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kumalizika, Simba imewatema Komambil Keita wa Mali, Danniel Akuffo wa Ghana na Pascal Ochieng wa Kenya.
Mjumbe mmoja wa Kamati hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema jana kwamba, wanatarajia kuwapata wachezaji hao kupitia michuano ya Chalenji inayoendelea nchini humo ikishirikishisha miamba 11 ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, pia Malawi iliyoalikwa.
Alisema, anaamini lengo lao litafanikiwa kutokana na ukweli kwamba, wachezaji wote wazuri wanaotoka katika nchi hizo, ndiyo waliyomo kwenye vikosi vya timu zao za Taifa zinazoshiriki michuano hiyo.
“Tumeona baadhi yetu waende Uganda kwenye Chalenji ili kusaka wachezaji watatu wa kimataifa watakaoziba pengo la kina Keita, Ochieng na Akuffo, kwani huko kutakuwa na wachezaji wengi wazuri,” alisema.
Kiongozi huyo aliongeza kwamba, kwa upande wa wachezaji wa ndani, tayari wameishaanza mazungumzo na baadhi ya nyota wanaotarajia kuwasajili katika dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufungwa Desemba 15.
“Hatuwezi kusema idadi kamili ya wachezaji wapya wa ndani tutakaowasajili, kwani mpaka sasa kuna mjadala juu ya suala hilo, kuna wengine watapelekwa kwa mkopo, kuna wengine tutabadilishana na baadhi ya timu,” aliongeza.
Kwa sasa, Simba imebakiza wachezaji wawili tu wa kigeni, Mganda Emmanuel Okwi na Mzambia Felix Sunzu.
Aidha, Simba ipo katika mazungumzo na wachezaji kadhaa wakiwemo Mkenya Jerry Santo anayekipiga Coastal Union ya Tanga, Juma Seif ‘Kijiko’ wa Yanga, huku pia ikiwa katika mpango wa kubadilishana wachezaji na Azam Fc.

Comments